Michezo

Mpe kazi Mourinho anyanyue Arsenal

November 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA JOB MOKAYA 

JOSE Mourinho amehusishwa na kumrithi Unai Emery huku matokeo ya Arsenal yakizidi kudidimia. Mourinho amekuwa kwenye kibaridi baada ya kupigwa kalamu na Manchester United mwaka mmoja uliopita.

Mourinho ana ari na moyo wa kurudi kazini huku akipendelea kuongoza timu iliyo katika ligi ya Uingereza akilenga kuwa binadamu wa kwanza kushinda mataji muhimu makuu katika timu tatu tofauti kwenye ligi ya Uingereza.

Ingawa Mourinho anamezea mate klabu yake ya zamani Real Madrid, anasema atahiari kujiunga na timu ya Uingereza kama itakuwa nafasi nzuri. Timu ambazo anaweza kujiunga nazo hivi sasa ni Arsenal na Tottenham.

Dalili za Unai kuweza kuimarisha Arsenal tangu achukue uongozi miezi 18 iliyopita hazipo. Na ni kukosekana kwa uwezekano huo ambapo sasa tetesi zinazagaa kila mahali kwamba Mourinho yu tayari kuchukua uongozi wa kuifunza Arsenal.

Wazo la Mourinho kuchukua mikoba ya kuiongoza Arsenal ni la ajabu na la kuwashangaza wengi. Mourinho tayari alikwisha haribu uhusiano wake na Chelsea pale ambapo aliamua kuiongoza Manchester United, na sasa ananuia kufanya hivyo akiwa na Arsenal.

Mourinho ameweka wazi kwamba yu tayari kujiunga na Arsenal endapo Unai atamwagishwa unga. Inaaminika kwamba timu ya Arsenal haina nia yoyote ya kumfuta Unai ila endapo matokeo yatazidi kuwa mabovu kiasi hiki basi mambo yatabadilika.

Basi endapo hali itabaki hivyo naye Jose Mourinho apewe nafasi ya kuiongoza Arsenal, ni nani atanufaika kutokana na uteuzi wake?

Wa kwanza kufaidika atakuwa kiungo wa kati Mezut Ozil. Ni bora kutaja kwamba Mezut Ozil na Mourinho hawakuwa na uhusiano mzuri enzi zao za Real Madrid. Ozil aliandika kwenye kitabu chake kuwa Mourinho alimwita ‘Mwoga’.

Hata hivyo, Ozil alitamba sana akicheza chini ya Mourinho na kuna uwezekano mkubwa kwamba hilo litatokea endapo The Special One atapewa nafasi ya kuiongoza Arsenal. Kwa sasa, Ozil hapati nafasi nyingi za kucheza.

Ni Jose Mourinho pekee anayeelewa kinagaubaga ubora na udhaifu wa Ozil. Ni Mourinho ajuaye kipaji na kipawa cha Ozil. Endapo wataungana tena katika uga wa Emirates, basi Ozil mwenye miaka 31 atarejelea tena usogora wake wa kupepeta gozi la mbuzi lililowambwa na kutengeneza mpira.

Mwingine atakayenufaika pakubwa na ujio wa Mourinho ni mshambulizi Pierre-Emerick Aubameyang huku Mourinho akipendelea acheze upande wa kushoto. Hapo, atafunga mabao mengi zaidi ya afanyavyo sasa hivi.

“Ninadhani kuwa Aubameyang anapendelea kucheza katikati ya uwanja kwa sababu anahisi kwamba anaweza kutinga magoli mengi. Lakini huenda akafunga magoli mengi zaidi endapo atacheza wingi ya kushoto,” Mourinho aliambia kituo kimoja cha runinga.

Mwingine anayeweza kunufaika na ujio wa Mourinho ni iwapo anaweza kumsajili Mouraine Fellaini. Fellaini alikuwa mchezaji muhimu katika timu ya Mourinho kwenye safu ya ukabaji uwanjani Old Trafford. Ingawa mashabiki wengi walimchukia Fellaini, ni Mourinho aliyejua umuhimu wake.