Mshambuliaji Jesse Were na Wakenya wenzake kurejea uwanjani kwa ligi ya Zambia Julai 18
Na GEOFFREY ANENE
LIGI Kuu ya Soka ya Zambia, ambamo karibu Wakenya 10 wanasakata soka yao ya malipo, imeratibiwa kurejea Julai 18, 2020.
Taarifa kutoka Shirikisho la Soka Zambia (FAZ) ilisema Juni 27 kuwa ligi hiyo inaweza kurejea Julai bora tu masharti makali kutoka kwa Wizara ya Afya ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona yazingatiwe.
Shirikisho hilo litakuwa na mkutano muhimu hapo Juni 30 na Julai 2 kujadiliana na klabu za Ligi Kuu na zile kutoka Ligi ya Daraja ya Pili baada ya kupata mwangaza huo wa kurejea viwanjani kutoka kwa Rais Edgar Lungu.
Katibu wa FAZ, Adrian Kashala amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Zambia akisema kuwa mazoezi ya vikundi vidogo vya wachezaji yanaweza kuanza Julai 1 wakifuata maagizo watakayopewa.
“Klabu za kutoka mikoa ya Lusaka, Central na Southern zitakutana mnamo Juni 30, huku zile kutoka Kaskazini, Kaskazini Magharibi na mkoani Copperbelt zikikusanyika Julai 2,” alisema afisa huyo, ambaye pia alishauri timu ziwasiliane na wasimamizi wa afya katika wilaya zao kufanya mipango ya wachezaji na maafisa kupimwa virusi hivyo ambavyo vimeua watu 21 nchini Zambia, 141 nchini Kenya na 501,868 kote duniani.
Mechi za ligi ya Zambia zitachezwa katika viwanja bila mashabiki kuzuia uenezaji wa virusi hivyo.
Baadhi ya Wakenya wanaotandaza soka yao nchini Zambia ni beki David ‘Calabar’ Owino, kipa Ian Otieno na washambuliaji Jesse Were na John Makwata (Zesco United), mabeki Musa Mohammed na Harun Shakava na viungo Duncan Otieno (Nkana) na Andrew Tololwa (Red Arrows).