Michezo

Mshindi wa EPL ni hadi siku ya mwisho – Klopp

April 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool anaamini kwamba kikosi chake kina uwezo wa kutwaa ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu iwapo vijana wake watashinda michuano yote minne inayowasubiri.

Ingawa hivyo, Liverpool watafikia tu ufanisi huo iwapo wapinzani wao wakuu Manchester City watajikwaa katika mojawapo ya mechi zao tano zilizosalia.

Baada ya kuwapepeta Chelsea kwa mabao 2-0 uwanjani Anfield, Liverpool walirejea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 85, mbili zaidi kuliko Man-City ambao wana michuano mitano zaidi ya kusakata muhula huu.

Awali, wachezaji Raheem Sterling na Gabriel Jesus walikuwa wamewaweka Man-City uongozini baada ya kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Crystal Palace uwanjani Selhurst Park.

Mabao ya Liverpool dhidi ya Chelsea yalifumwa wavuni na Sadio Mane na Mohamed Salah mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kati ya mechi nne ambazo Liverpool wamesalia nazo msimu huu, ni ile ya mwisho ambayo itawakutanisha na Wolves katika siku ya mwisho ya msimu ndiyo watakayoipiga nyumbani.

Baada ya kuvaana kesho Jumatano na FC Porto katika marudiano ya UEFA nchini Ureno, Liverpool wameratibiwa kupepetana na Cardiff City.

Wamepangiwa baadaye kumenyana na Huddersfield, Newcastle United na Wolves kwa usanjari huo.

Kwa upande wao, Man-City ambao wanafukuzia jumla ya mataji manne msimu huu, wameratibiwa kuchuana na Man-United, Burnley, Leicester City na Brighton mtawalia katika ligi.

Masogora hao wa kocha Pep Guardiola watachuana kesho na Tottenham uwanjani Etihad wakitarajia kubatilisha ushindi wa 1-0 uliovunwa na vijana hao wa Mauricio Pochettino ugani Wembley wiki jana.

Baada ya kuwakomoa Chelsea na kutua kapuni ufalme wa Carabao Cup mnamo Machi, Man-City kwa sasa wanawania taji la EPL, ubingwa wa UEFA na Kombe la FA. Watamenyana na Watford katika fainali ya Kombe la FA mnamo Mei 18.

Raheem Sterling alifunga mabao mawili na kuwasaidia waajiri wake Man-City kuwapepeta Crystal Palace 3-1 hapo jana katika mechi ya EPL ugani Selhurst Park.

Ushindi huo wa Man-City ambao bado wanafukuzia jumla ya mataji manne katika kamp- eni za muhula huu, ulikuwa wao wa tisa kusajili kwa mpigo katika kivumbi cha EPL.

Sterling afunga bao

Sterling aliwafungulia Man-City ukurasa wa mabao katika dakika ya 15 kabla ya kukiyumbisha kabisa chombo cha wenyeji wao kwa kupachika wavuni goli la pili katika dakika ya 63.

Goli la kwanza la Sterling lilikuwa zao la ushirikiano wake na kiungo mzaliwa wa Ubelgiji, Kevin De Bruyne aliyemzidi maarifa kiungo Patrick van Aanholt wa Palace.

Ushirikiano mkubwa kati ya Sterling na Leroy Sane ulichangia bao la pili la Man-City ambao kwa sasa wanapigiwa upatu wa kutetea kwa mafanikio ufalme wa taji la EPL.

Mbali na kuwania fursa hiyo ya kihistoria, Man-City pia wanafukuzia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Tayari wametawazwa mabingwa wa Carabao Cup baada ya kuwachabanga Chelsea kwenye fainali iliyowakutanisha Machi 2019.

Palace ambao kwa sasa wana alama 11 juu ya mduara wa kuteremshwa ngazi, walifutiwa machozi na Luka Milivojevic kunako dakika ya 81.

Hata hivyo, chombo chao kilizamishwa zaidi na Gabriel Jesus aliyewafungia Man-City bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili.