MSIHOFU: Je, Indomitable Lions itaweza kuipapura Benin?
Na MASHIRIKA
CAIRO, Misri
KOCHA wa Cameroon, Clarence Seedorf anatumai mabingwa hawa watetezi watapata matokeo ya kuridhisha zaidi watakapokuwa mawindoni dhidi ya Squirrels ya Benin katika kipute cha Kombe la Afrika (AFCON) leo Jumanne uwanjani Ismailia nchini Misri.
Indomitable Lions ilikabwa 0-0 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Black Stars ya Ghana ambayo ilikosa msisimko.
“Huenda mechi yetu ya kwanza haikuvutia kwa mashabiki ila tunataka kufanya vyema zaidi. Hata hivyo, niliona timu iliyojipanga na kuunda nafasi nyingi zilizostahili kuzalisha ushindi,” alisema Seedorf.
Seedorf alitetea mbinu zake baada ya kutofikia matarajio dhidi ya Ghana akisema kuwa kila mara lengo lake huwa ni kuibuka na ushindi.
“Hatuanzi mechi kupata sare, tunaianza kupata ushindi, lakini nilitosheka na alama tuliyopata,” alisema kuhusu matokeo hayo ambayo yanaweka Cameroon katika nafasi nzuri ya kuingia mduara wa 16-bora. Cameroon inaongoza Kundi F kwa alama nne, mbili zaidi ya Benin na Ghana na tatu kuliko Guinea-Bissau.
Benin inatafuta ushindi wa kwanza kwenye kombe hili baada ya kuambulia sare mbili katika matokeo yake mazuri tangu ishiriki mara ya kwanza mwaka 2004. Ilipata pigo katika juhudi zake za kuandikisha ushindi ilipokabwa 0-0 dhidi ya Guinea-Bissau.
Shujaa wa soka ya Afrika, Jay-Jay Okocha anaamini kuwa kocha wa Ghana, Kwesi Appiah huenda akapigwa kalamu vijana wake wakilimwa na Guinea-Bissau na kuaga mashindano.
Kiungo huyu mstaafu kutoka Nigeria anasema “amesikitishwa na Appiah jinsi wanavyohisi Waghana” baada ya sare dhidi ya Benin na pia Cameroon ambazo hazijahakikishia Black Stars tiketi ya kusonga mbele.
“Kwesi lazima ashinde Guinea-Bissau kuhifadhi kazi yake,” alisema Okocha ambaye alikuwa katika kikosi cha Nigeria kilichotwaa kombe hili mwaka 1994.
Guinea-Bissau ni mojawapo ya timu nne ambazo hazijapata bao, huku mshambuliaji wa zamani wa akademia ya Liverpool Toni Silva akiwa katika orodha ya walio butu.
Kundi hili lingali wazi kwa washiriki wote wanne kunyakua tiketi mbili za moja kwa moja zilizoko mezani sawa na Kundi E linalojumuisha Mali, Tunisia, Angola na Mauritania.
Mali na Angola zilisisimua mashabiki katika mechi ya ufunguzi ya AFCON mwaka 2010. Katika mechi hiyo iliyotamatika 4-4, Mali ilifungwa na wenyeji Angola mabao manne ndani ya dakika 74 kabla ya kurejesha yote katika dakika za lala-salama. Mataifa haya yana fursa nyingine ya kuonyesha ukatili wao mbele ya lango yatakapolimana leo.
Mmoja wa wachezaji Mali itategemea ni Moussa Marega, ambaye mabao yake sita katika timu ya Porto kwenye Klabu Bingwa Ulaya yalimweka katika nafasi ya tatu katika ufungaji nyuma ya nyota wa Argentina Lionel Messi na raia wa Poland Robert Lewandowski.
Angola hawajakuwa rahisi kutabirika baada ya kuambulia sare mbili chini ya kocha Srdjan Vasiljevic kutoka Serbia, waliporidhisha wakigawana alama na mabingwa wa mwaka 2004 Tunisia kabla ya kusikitisha katika sare nyingine dhidi ya washiriki wapya kabisa Mauritania.
Kusikitisha
Tunisia wanaongoza orodha ya miamba waliosikitisha zaidi katika makala haya ya 32 kufikia sasa kwa kuambulia alama mbili kutokana na mechi zake dhidi ya Angola na Mali.
Kocha Alain Giresse amejibu wakosoaji wake kwa hasira kuhusu kutomwanzisha kiungo Ferjani Sassi.
“Ferjani anarejea kutoka mkekani na anahitaji muda mzuri wa kupona kabisa ili afikie hali nzuri,” Mfaransa huyo alisema.
Baada ya kulimwa 4-1 na Mali katika mechi ya ufunguzi, Mauritania walijikakamua na kulazimisha sare tasa dhidi ya Angola na watatumai kusajili ushindi wa kwanza dhidi ya Tunisia inayojivunia kuwa na mshambuliaji hodari Wahbi Khazri.