Michezo

Msusi Sharon Bitok alenga dhahabu za mbio za 800m na 1,500m kwenye Olimpiki za Viziwi

Na GEOFFREY ANENE November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHARON Bitok alipojitokeza kwa mara ya kwanza kimataifa katika Michezo ya Dunia ya Watu Wenye Ulemavu wa Kusikia maarufu kama Deaflympics mwaka 2021 mjini Lublin, Poland, alimaliza miongoni mwa washiriki wa mwisho katika mbio za wanawake za mita 800 na 1,500.

Hata hivyo, chini ya mwaka mmoja baadaye, Bitok alirejea kwa kishindo katika Deaflympics 2022 mjini Caxias do Sul, Brazil, ambapo alishinda medali tatu za fedha katika 800m, 1500m na mbio za kupokezana vijiti za 4x400m.

Akielekea kwenye Deaflympics 2025 jijini Tokyo, Bitok,29, kutoka Iten mjini Eldoret, amedhamiria kutwaa dhahabu, si kwa heshima ya taifa pekee, bali pia kuboresha maisha ya familia yake.

“Nikiwa Poland nilikuwa na uoga na pia bila uzoefu, lakini nilipofika Brazil nilikuwa na ujasiri na nikashinda fedha tatu. Wakati huu, nataka dhahabu ya 800m na pia 1500m,” alisema Bitok, mmoja wa wanariadha 31 waliotunukiwa katika sherehe za Mashujaa Day za 2024 mjini Kitui.

Ili kuongeza nafasi zake, mama huyo wa mtoto mmoja ameimarisha mazoezi ya kasi kwa ajili ya 800m, huku akiboresha uvumilivu kwa 1,500m. “Nimepata hamasa na najihisi nina uwezo wa kuwashinda wapinzani wangu. Wenzangu wa Ulaya wana vifaa bora, lakini nimefanya maandalizi ya kutosha. Tukutane uwanjani,” alisema kwa kujiamini Ijumaa, Novemba 7, 2025.

Mtaalamu huyo wa ususi kutoka Eldoret atawakilisha Kenya kwenye mbio za 800m akishirikiana na Aidah Odero, na katika 1,500m akishirikiana na Viola Chelimo na Rebecca Matiko. Wakiwa na makocha Sammy Kibet na Caroline Kola, wameandaa mikakati mahsusi ya kuhakikisha Kenya inang’aa.

Zaidi ya medali, Bitok anapata motisha kutokana na zawadi za fedha kwa washindi wa Deaflympics zilizotangazwa hivi karibuni na Rais William Ruto. “Nataka kushinda dhahabu nipate zawadi ya Sh3 milioni ili niweze kumtunza mwanangu na kuimarisha maisha yetu,” akaapa Bitok anayemuenzi bingwa wa dunia wa 1,500m Faith Kipyegon.