Michezo

MTAISOMA NAMBA: Mo Farah aonya washindani wake mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki za Tokyo

May 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MWANARIADHA mahiri mzawa wa Somalia na raia wa Uingereza, Mohamed Muktar Jama almaarufu Mo Farah, amesema yuko tayari kuwaonyesha wapinzani wake kivumbi katika michezo ijayo ya Olimpiki.

Farah ndiye mtimkaji anayejivunia ufanisi mkubwa zaidi katika ulingo wa riadha kwenye historia ya taifa la Uingereza.

Amethibitisha kwamba atashuka ugani kuwania nishani ya dhahabu katika mbio za 10,000m jijini Tokyo, Japan michezo hiyo itakapoandaliwa mwakani.

Olimpiki za Tokyo ziliahirishwa mwaka 2020 kutokana na janga la corona ambalo limetatiza pakubwa ulingo wa michezo duniani kote.

Farah alistaafu miaka miwili iliyopita na akajibwaga katika mbio za masafa marefu za marathon, ambako hajafanikiwa kujinyakulia nishani yoyote.

Mwanariadha huyo aliambulia nafasi ya nane katika kivumbi cha Chicago Marathon, aERIKA mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2019.

Michezo ijayo ya Olimpiki itampa Farah jukwaa maridhawa la kutia kibindoni nishani ya 11 ya dhahabu katika historia ya kushiriki kwake mbio za mita 10,000.

“Ninatawaliwa na hamu pamoha na kiu ya kutetea ufalme wa mbio za mita 10,000 jijini Tokyo, Japan. Nimekuwa nikishiriki mazoezi ya kuboresha kasi yangu na ninahisi kwamba mwili wangu kwa sasa uko shwari na tayari kuwabwaga wapinzani wangu,” akasema.

Farah, 36, anajivunia dhahabu nne za Olimpiki baada ya kutawala mbio za mita 5,000 na 10,000 katika makala yaliyopita ya London, Uingereza (2012) na Rio, Brazil (2016).

Tangu 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala fani yam bio za mita 5,000 kwa wanaume katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 ambazo zimekuwa zikitawaliwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Mo Farah.

Rekodi ya Kenya katika mbio hizo hata katika michezo ya Olimpiki haijakuwa ya kuridhisha, katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kujizolea medali ya dhahabu katika mbio hizo kwenye Olimpiki za 1988 zilizoandaliwa jijini Seoul, Korea Kusini.

Wakenya wanaotazamiwa kutoana kijasho na Mo Farah katika mbio za mita 10,000 jijini Tokyo, Japan mwaka 2021 ni Geoffrey Kamworor, Alex Oloitiptip, Rhonex Kipruto na Rodgers Kwemoi aliyeibuka mfalme wa dunia kwa vijana wasiozidi miaka 20 mnamo 2016.