Mtembeaji Gathimba akosa Sh6.4 milioni akimaliza nambari 22 Olimpiki
BINGWA wa zamani wa Afrika wa kutembea haraka kilomita 20 Samuel Gathimba, Alhamisi aliambulia pakavu katika vita vya kuwania tuzo ya Sh6.4 milioni (Dola za Amerika 50,000) anazopata mshindi katika riadha kwenye Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.
Afisa huyo kutoka Idara ya Magereza amekamata nafasi ya 22 kwa saa 1:21:26 kati ya washiriki 49, huku Brian Pinado (Ecuador), Caio Bonfim (Brazil) na bingwa wa dunia Alvaro Martin (Uhispania) wakifagia medali kwa 1:18:55, 1:19:09 na 1:19:11 mtawalia katika usanjari huo.
Gathimba anajivunia medali tatu za dhahabu kutoka Riadha za Afrika na moja katika Michezo ya Afrika pamoja na fedha mbili za Michezo ya Afrika na moja kwenye Riadha za Afrika na shaba moja ya Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Muda wake bora mwaka huu kabla ya Olimpiki ulikuwa 1:28:06 kumaanisha aliuimarisha, lakini hiyo haikutosha hata kuwa karibu na mduara wa medali.
Gathimba alishiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza mjini Rio de Janeiro nchini Brazil mwaka 2016, lakini hakumaliza mashindano.
Alikosa makala yaliyopita mjini Tokyo nchini Japan mwaka 2021 kwa njia ya kutatanisha kabla ya kufuzu kushiriki makala haya ya 33.
Hakuna Mwafrika amewahi kuibuka mfalme wa kutembea kwa haraka kwenye Olimpiki tangu fani hiyo ijumuishwe kwa mara ya kwanza mwaka 1956.
Mbali na Gathimba, Wakenya wengine wanaume waliojaribu bahati katika fani hiyo ya kutembea kwa haraka katika Olimpiki, ni Pius Munyasia mjini Los Angeles nchini Amerika mwaka 1984, na David Kimutai, Justus Kavulanya na Julius Sawe mjini Atlanta nchini Amerika mwaka 1996.
Kimutai na Sawe pia walishiriki makala ya Sydney nchini Australia mwaka 2000. Isitoshe, Kimutai alishiriki makala ya 2008 mjini Beijing, Uchina naye Simon Wachira hakumaliza mbio mwaka 2016.
RATIBA YA OLIMPIKI AGOSTI 2:
11.35am – michujo ya 100m (wanawake)
12.10pm – michujo ya 1,500m (wanaume)
7.10pm – michujo ya 5,000m (wanawake)
8.10pm – 4x400m (mseto)
8.45pm – michujo ya 800m (wanawake)
10.00pm – fainali (wanaume)