• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Mtihani mkali wawasubiri Chipu katika raga ya dunia

Mtihani mkali wawasubiri Chipu katika raga ya dunia

Na GEOFFREY ANENE

CHIPU, ambayo ni timu ya Kenya ya raga ya wachezaji chipukizi, ina kibarua kigumu itakapomenyana na Uruguay katika mechi yake ya ufunguzi ya Raga ya Dunia ya Under-20 Trophy leo Jumanne saa tano usiku mjini Sao Paulo nchini Brazil.

Mabingwa hawa wa Bara Afrika wanarejea katika jukwaa hili la dunia baada ya kuwa nje miaka 10. Walimaliza katika nafasi ya nne waliposhiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa wakiwa wenyeji mwaka 2009 jijini Nairobi.

Vijana wa kocha Paul Odera watatumai kuwa na mwanzo mzuri dhidi ya wapinzani hao kutoka Amerika Kusini, ambao wana uzoefu mwingi katika mashindano haya ya daraja ya pili.

Tofauti na Kenya, ambayo inashiriki mashindano haya kwa mara ya pili katika historia yake, Uruguay imekuwa katika mashindano haya miaka tisa pamoja na kutwaa taji la mwaka 2008. Pia, majirani hawa wa Brazil walishiriki mashindano ya daraja ya juu kabisa mwaka 2009.

Chipu ilikuwa katili ikijikatia tiketi ya kuelekea Brazil pale ilipokung’uta Tunisia kwa alama 73-0 katika nusu-fainali ya Barthes Trophy mnamo Aprili 4 na kuduwaza miamba Namibia 21-18 katika fainali jijini Nairobi mnamo Aprili 7.

Odera na vijana wake walisherehekea kuandiisha historia hiyo ya kupiga Namibia kwa mara ya kwanza kabisa kwa kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu.

Hata hivyo, mashindano ya dunia ni kiwango tofauti sana na ya Bara Afrika na watakutana na mataifa yanayoorodheshwa juu ya Kenya kwenye viwango vya ubora vya raga duniani katika Kundi “A”. Japan inashikilia nafasi ya 11, Uruguay ni ya 19 nayo Brazil iko katika nafasi ya 26.

Kenya ni nambari 32 duniani, kumaanisha itahitaji kufanya kazi ya ziada kukwepa vichapo vya aibu.

Timu yakosa matayarisho muhimu

Chipu ilikosa matayarisho iliyoyataka kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Haikuenda nchini Afrika Kusini kwa kambi ya mazoezi maalumu, ambako pia ilitarajia kucheza mechi kadhaa za kirafiki.

Vijana wa Odera walilazimika kujipima nguvu dhidi ya timu iliyoundwa kutoka ligi ya Shule za Upili almaarufu Prescott Cup na pia timu mbili zilizokuwa zikijaribiwa wakati wa kuchagua timu ya taifa ya watu wazima almaarufu Simbas.

Wakenya pia hawakupata makocha wawili maalum kutoka Afrika Kusini kutokana na notisi ya muda mfupi waliopewa kuja Nairobi.

Licha ya changamoto hizi, Odera anasalia na matumaini makubwa kuwa Kenya itakamilisha mashindano haya ya Julai 9-21 katika nafasi ya kuheshimiwa.

Akitaja kikosi cha mwisho jijini Nairobi mnamo Juni 26, Odera alisema kuwa lengo la Chipu ni kukamilisha mechi za kundi lake katika nafasi ya pili. Hata hivyo, alikiri,

Timu za Tonga, Ureno, Canada na Hong Kong ziko katika Kundi “B”. Zinakamilisha orodha ya washiriki walio mjini Sao Paulo kuwania tiketi moja ya kuingia mashindano ya daraja ya juu kujaza nafasi ya Scotland, ambayo imeshushwa ngazi baada ya kuvuta mkia Argentina mwezi uliopita.

  • Tags

You can share this post!

Vipusa wa USA watetea ubingwa wa Dunia gozini

Uhuru akwepa Mlima Kenya

adminleo