• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Mulee aita Makwatta kujaza pengo la Olunga

Mulee aita Makwatta kujaza pengo la Olunga

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI John Mark Makwatta anayechezea Zesco United ya Zambia ameitwa kambini mwa Harambee Stars wanaojiandaa kuvaana na Comoros kwenye mechi mbili zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Chini ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee, Stars wamepangiwa kuvaana na Comoros katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Novemba 11, 2020 uwanjani Nyayo kabla ya kurudiana na Wanavisiwa hao simu nne baadaye jijini Moroni.

Kuitwa kwa Makwatta ambaye ni mchezaji wa zamani wa Ulinzi Stars kulichochewa na haja ya Mulee kujaza pengo la mshambuliaji Michael Olunga anayepigia Kashiwa Reysol ya Japan.

Kikosi kizima cha Reysol kinachoshiriki Ligi Kuu ya Japan (J1 League) kililazimika kutiwa karantini baada ya watu watano kambini mwao kuugua Covid-19.

Kukosekana kwa Olunga kulitusukuma kutafuta mfumaji mbadala. Tulihisi kwamba Makwatta ndiye anayestahili zaidi kuwa kizibo cha Olunga. Ana tajriba pevu na uzoefu mkubwa katika ulingo wa soka ya kimataifa. Isitoshe, analeta pia ushindani mzuri katika safu ya mbele ya Stars,” akasema Mulee.

“Nina furaha kubwa kurejea kambini mwa Stars. Niko katika fomu nzuri na nitapania kujituma zaidi dhidi ya Comoros na kushindia Stars mechi mbili muhimu zijazo kwenye safari ya kufuzu kwa AFCON,” akasema Makwatta ambaye alichezea Stars mara ya mwisho mnamo 2018 kwenye kipute cha Hero Cup nchini India.

Nyota huyo aliyetawazwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2016, aliripoti kambini mwa Stars mnamo Novemba 9, 2020 kwa pamoja na wanasoka wenzake wa Zesco United – Ian Otieno na David ‘Calabar’ Owino.

Makwatta anatazamiwa kushirikiana na Benson Omala (Gor Mahia), Masoud Juma (JS Kabylie, Algeria), John Avire (Tanta SC, Misri) na Oscar Wamalwa (Ulinzi Stars, Kenya) kwenye safu ya mbele ya Stars.

Wachezaji wengine wanaosakata kabumbu ya kulipwa ughaibuni ambao walijiunga na Stars mnamo Novemba 9 ni Brian Mandela (Mamelodi Sundowns, Afrika Kusini), Eric Johanna (J-Sodra, Uswidi), Joseph Okumu (Elfsborg, Uswidi) na Anthony ‘Teddy’ Akumu (Kaizer Chiefs, Afrika Kusini).

Wengine ni Ismael Gonzalez (Las Palmas, Uhispania), Masoud Juma (JS Kabylie, Algeria), Avire (Tanta SC, Misri) na Ayub Timbe ambaye bado hana klabu tangu aagane na Beijing Renhe ya China mnamo Oktoba 2020.

Mathew Olaka aliyewahi kuchezea Lakehill FC ya Canada alitemwa katika kikosi cha sasa kinachoshiriki mazoezi uwanjani MISC Kasarani baada ya kushindwa kuridhisha benchi ya kiufundi inayoongozwa na Mulee pamoja na Twahir Muhiddin na kocha mkuu wa Bandari FC, Ken Odhiambo.

  • Tags

You can share this post!

Ubunifu wa mitego maalum unavyomsaidia kurina asali

Wakenya washinda Istanbul Marathon