Michezo

Mulee awaita Juma na Masika kikosini

November 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jacob ‘Ghost’ Mulee amefichua kikosi cha Harambee Stars kitakachovaana na Comoros jijini Moroni mnamo Novemba 15 kwenye marudiano ya kipute cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Stars ambao wamesajili sare tatu kutokana na michuano mitatu iliyopita ya Kundi G, wanaelekea Comoros wakiwa na ulazima wa kutia kapuni alama zote tatu ili kuweka hai matumaini ya kufunga safari ya kuelekea Cameroon kwa minajili ya AFCON mwaka ujao.

Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi chini ya mkufunzi Francis Kimanzi.

Katika kibarua chake cha kwanza kambini mwa Stars tangu aaminiwe kuwa mrithi wa Kimanzi mnamo Oktoba 21, 2020, Mulee aliwaongoza vijana wake kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Comoros mnamo Novemba 11, 2020 ugani MISC Kasarani. Stars waliondoka humu nchini mnamo Novemba 14 asubuhi wakiwa wameabiri ndege ya kibinafsi.

Mulee atapania kutegemea hudua za wanasoka waliocheza dhidi ya Comoros mnamo Novemba 11 baada ya kudumisha kikosini kikosi kizima kilichonogesha gozi hilo la mkondo wa kwanza.

Hata hivyo, amemjumuisha kiungo mpya wa Sofapaka, Lawrence Juma kwenye kikosi chake baada ya nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia kukosa fursa ya kudhihirisha uwezo wake ugani dhidi ya Comoros ugani MISC Kasarani.

Sura nyingine mpya katika kikosi cha wanasoka 25 ambao wamesafiri na Mulee nchini Comoros ni kiungo Musa Masika wa Wazito FC. Hatua ya Mulee kusafiri na wawili hao ni ishara kwamba anatazamia kukifanyia kikosi chake mabadiliko makubwa ili kicheze gozi la kubana na kuzuia sana ili Stars wasajili sare nyingine ugenini.

Anayekosekana katika kikosi cha Mulee ni beki wa zamani wa Gor Mahia, Joash Onyango ambaye kwa sasa huchezea Simba SC ya Tanzania. Licha ya Onyango kudaiwa kwamba anaugua Covid-19, usimamizi wa Simba umekanusha tetesi hizo na kusisitiza kwamba beki huyo matata alikosa mechi ya kwanza iliyokutanisha Stars na Comoros jijini Nairobi kwa sababu ya jeraha la mguu alilolipata kwenye gozi kati ya Simba na Yanga mnamo Novemba 7, 2020.

Licha ya kupoteza alama mbili muhimu dhidi ya Comoros nyumbani, Mulee ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi chake bado kina uwezo wa kuibuka na ushindi muhimu wa ugenini.

“Chochote kinawezekana katika soka. Tulijifunza mambo kadhaa dhidi ya Comoros nyumbani na kwa sasa tunajua cha kufanya jijini Moroni,” akasema Mulee katika kauli iliyoungwa mkono na kipa Arnold Origi wa HIFK Fotboll (Finland) anayerejea kambini mwa Stars kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano.

Origi atakuwa akiadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwake mnamo Novemba 15, 2020.

KIKOSI CHA STARS:

MAKIPA:

Arnold Origi, Ian Otieno, Brian Bwire

MABEKI:

Brian Mandela, Joseph Okumu, Samuel Olwande, Erick Ouma, David Owino Odhiambo, David Owino Ambulu, Johnstone Omurwa

VIUNGO:

Victor Wanyama, Johanna Omollo, Cliff Nyakeya, Ayub Timbe, Eric Johanna, Ismael Gonzalez, Anthony Akumu, Lawrence Juma, Boniface Muchiri, Musa Masika, Abdallah Hassan,

MAFOWADI:

Masud Juma, John Avire, Mark Makwatta