Michezo

Munyua afunguka kuhusu mchezo wa Darts

Na TOTO AREGE December 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKENYA David Munyua ameelezea kuwa safari yake ya ulengaji vishale kwa kimombo “darts”, umebadilisha maisha yake.

Jumatatu usiku, Munyua ambaye ni mkaazi wa Kaunti ya Murang’a, alipoteza 3-0 dhidi ya Kevin Doets (ameorodheshwa nafasi ya 38 duniani) kutoka Uholanzi katika raundi ya pili ya mashindano ya Kombe la Dunia la Ulengaji Vishale yanayoendelea London.

“Huu ni wakati wa kubadilisha maisha yangu na marafiki wangu na kwa wachezaji wa darts kote Afrika,” Munyua aliwaambia waandishi wa habari dakika chache tu baada ya kupoteza dhidi ya Doets.

Munyua 30, aligonga vichwa vya habari Alhamisi wiki jana, baada ya kumbwaga Mike De Decker (anayeshikilia nafasi ya 18 duniani) wa Ubelgiji 3-2 katika raundi ya kwanza.

Kufuzu kwake kwa raundi ya pili, alijinyakulia £25,000 (millioni 4.3) kama zawadi.

“Hii ni motosha kwa wale wote wanaohisi kwamba hawawezi. Kwa hivyo nadhani huu ndio wakati ambapo ninahitaji kuthamini ukweli kwamba Afrika inahitaji kukumbatia mchezo wa darts. Mchezo huu utabadilisha maisha,” aliongezea Munyua ambaye ni daktari wa mifugo.

Ushindi wa Munyua katika raundi ya kwanza ulimfanya Rais William Samoei Ruto, kumpongeza kwa ushindi.

Munyua alisisitiza matumaini yake ya kuwa amebadilisha mtazamo wa mchezo wa darts barani Afrika.

“Mchezo wa darts barani Afrika haujatambuliwa kama mchezo,” alisema. “Katika ngazi ya kitaalamu, hakuna mtu angetaka kupata zaidi katika mchezo wa darts kwa sababu haileti kitu chochote kutoka kwake.

“Nadhani tukikuza mchezo huu, kila mtu atataka kujiungA nao. Haijalishi taaluma walonayo. Hicho ndicho ninaamini kingekuwa muhimu sana kwangu. Tumefanya mengi. Tumejitolea sana. Mimi mwenyewe na taaluma yangu, nimejitolea sana,” aliongezea.

Hata hivyo, Munyua ambaye alikuwa mwakilishia wa Afrika katika shindano hilo, aliomba Shirika la Vishale (PDC) kuongeza idadi ya wanaofuzu kutoka Afrika na kuleta mashindano tofauti tofauti Afrika ili kukuza mchezo huo.