Michezo

Murunga ataja kikosi cha Shujaa kwa ajili ya London 7s, Fiji na Samoa pia zataja vikosi

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imekuwa timu ya hivi punde ya Kundi B kutangaza kikosi chake kitakachoshiriki duru mbili za mwisho za Raga ya Dunia katika miji ya London, Uingereza (Mei 25-26) na Paris, Ufaransa (Juni 1-2).

Kocha Paul Murunga amefanyia kikosi chake kilichozuru Bara Asia kwa duru za Hong Kong na Singapore mabadiliko manne Alhamisi.

Murunga, ambaye vijana wake wanshikilia nafasi ya 13 kwa alama 26, pointi nne juu ya Japan inayovuta mkia kwenye ligi hii ya mataifa 15 na timu moja alikwa, amejumuisha Jacob Ojee, Cyprian Kuto, Brian Wandera na Charles Omondi na kuacha nyumbani Augustine Lugonzo, Oscar Dennis, Shaddon Munoko na Mark Wandetto.

Ojee alikosa ziara ya Asia mwezi Aprili akifanya mtihani wake wa mwisho wa Digrii ya Msuala ya Kifedha katika Chuo Kikuu cha USIU jijini Nairobi nao Kuto, Wandera na Omondi wamepona majeraha. Jeffery Oluoch, ambaye aliteuliwa nahodha wa duru za Hong Kong na Singapore, atakuwa nahodha msaidizi katika ziara hii ya Bara Ulaya.

Katika siku ya kwanza ya London Sevens hapo Mei 25, Kenya italimana na nambari mbili duniani Fiji (12.36pm), nambari sita Samoa (3.20pm) na kukamilisha mechi za makundi dhidi ya nambari tisa Ufaransa (6.26pm).

Kocha Paul Murunga wa timu ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya katika hii picha ya awali. Picha/ Chris Omollo

Fiji ya kocha Gareth Baber ilitaja kikosi chake Mei 14 na kusafiri nchini Uingereza hapo Mei 15 siku ambayo Gordon Tietjens alitangaza kikosi cha Samoa.

Baber anakaribisha mchezaji mbunifu Waisea Nacuqu, ambaye aliumia bega wakati wa duru ya Las Vegas nchini Marekani mnamo mapema mwezi Machi, na Jerry Tuwai aliyekuwa akisumbuliwa na jeraha la mguu wakati wa Singapore Sevens.

Samoa ilipata tena huduma za Joe Perez aliyeumia wakati wa Vancouver Sevens nchini Canada mnamo Machi 9-10. Kocha Jerome Daret anatarajiwa kutangaza kikosi cha Ufaransa wakati wowote.

VIKOSI    

Kenya

Vincent Onyala, Andrew Amonde, Bush Mwale, Daniel Sikuta, Charles Omondi, Eden Agero, Daniel Taabu, Jacob Ojee (nahodha), Cyprian Kuto, Jeffery Oluoch, Nelson Oyoo, Johnstone Olindi, Brian Wandera

Fiji

Sevuloni Mocenacagi, Josua Vakurinabili, Isoa Tabu, Paula Dranisinukula (nahodha), Apenisa Cakaubalavu, Ratu Meli Derenalagi, Filimoni Botitu, Livai Ikanikoda, Jerry Tuwai, Alasio Naduva, Aminiasi Tuimaba, Waisea Nacuqu, Napolioni Ratu, Asaeli Tuivoka

Samoa

David Afamasaga (nahodha), Tomasi Alosio, Alamanda Motuga, Johnny Vaili, Joe Perez, Johnny Samuelu, Tila Mealoi, Siaosi Asofolau, Laaloi Leilua, Elisapeta Alofipo, Paul Scanlan, Phillip Luki, Melani Matavao, Paulo Toilolo Fanuasa