Michezo

Musa Otieno aingia ubia na BetLion kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi mashinani

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA wa zamani wa Harambee Stars, Musa ‘Otero’ Otieno ameingia ubia na kampuni ya BetLion kwa minajili ya kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi mashinani.

Otieno ambaye amewahi pia kuchezea AFC Leopards na Tusker zamani ikiitwa Kenya Breweries kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Santos FC nchini Afrika Kusini.

Baada ya kustaafu soka, alipokezwa mikoba ya kuwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kisha mkufunzi wa chipukizi.

Otieno ameteuliwa kuwa balozi wa mauzo wa huduma za BetLion kwa jamii baada ya kampuni hiyo ya mchezo wa Kamari kufichua azma ya kushirikiana na wadau wa soka kukuza talanta za vijana humu nchini.

Kati ya miradi itakayoendeshwa na BetLion ni kuzuru maeneo mbalimbali ya humu nchini na kutambua vikosi vilivyopo mstari wa mbele kukuza vipaji vya chipukizi. Vikosi vya aina hiyo vitapokezwa vifaa vya mchezo kwa hisani ya BetLion na kuwezeshwa kifedha.

“Tuliteua Musa Otieno kuongoza mradi huu kwa sababu ni kielelezo kwa wanasoka wengi chipukizi,” akasema Mkurugenzi Msimamizi wa BetLion, Spencer Okach.

Otieno ni miongoni mwa wanasoka wanaojivunia utajiri mkubwa wa talanta na nidhamu ya juu zaidi kutoka humu nchini katika enzi yake.

“Aliwahi kuvalia jezi za AFC Leopards na Tusker kabla ya kujiunga na Sanlam Santos FC ya Afrika Kusini alikohudumu kwa zaidi ya kipindi cha miaka 10 akiwa mchezaji kabla ya kujitosa katika ulingo wa ukocha,” akaongeza.

Alivalia utepe wa unahodha wa Harambee Stars katika fainali za Kombe la Afrika mnamo 2004 nchini Tunisia. Kikosi cha Kenya wakati huo kilikuwa kikijivunia wanasoka wa haiba kubwa wakiwemo Dennis Oliech, Mike Okoth, Titus Mulama na Robert Mambo.

Baada ya kustaafu soka, Otieno aliaminiwa kuwa msaidizi wa Harambee Stars chini ya wakufunzi Bobby Williamson na Stanley Okumbi. Awali, alikuwa pia katika benchi ya kiufundi ya timu ya taifa ya wanawake, Harambee Starlets. Otieno kwa sasa ni mchanganuzi wa masuala ya spoti katika redio na runinga za humu nchini.