Michezo

Mutomo Youth yajinyanyua baada ya kusambaratika

August 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PATRICK KILAVUKA

MUTOMO Youth kutoka kaunti ndogo ya Gatundu Kusini ilibuniwa baada ya timu ya Gatundu Stars kukosa ufadhili na kusambaratika baada ya wadhamini Kenya Clay and Trax kujiondoa.

Vijana hawa chipukizi ambao walikuwa wanalelewa na timu ya Stars wakiwa U-18 waliwaza na kuwaza jinsi ya mbegu ya soka ambayo ilikuwa imepandwa na watangulizi ingenyunyiziwa ili iendelee kustawishwa kwani, wanasoka wazamani walisaka majani mabichi katika timu zingine na wengine kwa sababu za kiajira wakawa wanahamia pembe zingine za nchi.

Kikosi cha Mutomo FC ( jezi ya manjano na miraba ya buluu) kutoka kaunti ndogo ya Gatundu Kusini kikishauriwa na kocha wao. Picha/Patrick Kilavuka  

Wazo lao lilizaa matunda kwani timu ya Youth ilibuniwa kuendelea kupeperusha bendera ya kabumbu eneoni kwa kujituma wakitumiania kwamba, wadau wakuu eneoni watagusiwa kuisaidia kuwapelekea kufikia ndoto zao katika ulimwengu wa soka.

Japo kufikia sasa hamna udhamini wowote umejitokeza ila, kuna uhisani tu wa kutoka kwa wachezaji wenyewe, mashabiki na jamii ambayo inatoa kidogo kujaza kibaba cha timu kuendelea kugharamia matakwa ya timu hii ambayo inavumisha kandanda Kauntini.

Kikosi cha Mutomo FC kutoka Gatunda Kusini wakati kilipocheza na Mwimuto Wailers uwanjani Appproved, Lower Kabete. Picha/Patrick Kilavuka

Ni miaka mitatu tangu vijana hawa wa kutoka shule za eneo hilo kushikamana pamoja na kuazimia kukumbatia soka kufufua matumaini ya kukuza kandanda ya hadhi ambayo ilikuwa inasakatwa na timu ya Stars ambayo ilicheza hadi Daraja ya Pili ya ligi kuu nchini.

Wanasoka hawa ni wanafunzi wa zamani wa Shule za Upili za Kahogoini, Kimonyo, Muroria, Muhoho, Kijabe na Hisani. Walioistawisha walikuwa wachezaji 15 japo sasa wanaweza za kufika 20.

Kikosi cha Mutomo FC (jezi ya manjano na miraba ya bluu) kutoka kaunti ndogo ya Gatundu Kusini ambacho kinashiriki ligi ya FKF Kaunti ya Kiambu Tawi la Abardares wakicheza dhidi ya Mwimuto Wailers Jr uwanjani Approved, Lower Kabete. Picha/Patrick Kilavuka

Timu hii inafanyia mazoezi na kusakatia mechi zake za ligi Shule ya Msingi ya Mutomo na kwa muda imebuniwa imenawiri na kupanda ngazi baada ya nyingine katika ligi ya FKF wakiwa bingwa wa ligi ya kaunti ndogo ya Gatundu Kusini.

Mwaka wao wa kwanza (2016) kutia guu katika ligi hiyo, walimaliza tano bora jedwalini kabla kujishuka kwa mwaka jana na kupigana ukucha kwa jino na kuibuka kidedea baada ya kuicharaza timu ya Sisal FC 6-0 na kufuzu ligi ya Kaunti.

Katika mkumbo wa kwanza wamezoa alama 21 baada ya kupiga michauno kumi na mitano huku mechi za mwishomwisho ikionesha ni moto wa kuotewa mbali baada ya kuinyorosha Murera FC 4-1, kuinyeshea TNT Dyanmites 7-0 na kuizidi maarifa TCM kwa kuitandika 2-1 kabla kuagana sare tasa dhidi ya Mwimuto Wailers Jr ambayo ilikuwa kisiki chao ligini katika mechi iliyopigiwa uwanjani Approved, Lower Kabete.

Kikosi cha Mutomo FC kutoka kaunti ndogo ya Gatundu Kusini kikijinoa kabla kucheza mchuano wa dhidi ya Mwimuto Wailerd Jr. Picha/Patrick Kilavuka

Kando na kushiriki katika ligi, wametumbiza mashabiki wao katika ligi ya Chapa Dimba ingawa walibinywa na Mundoro FC 2-1 katika fainali za kaunti ndogo ya Gatundu Kusini.

Benchi ya timu ambayo inaongozwa na kocha Peter Mburu Kabubi, naibu mkufunzi Samuel Mbuthia, timu meneja Moses Muigai na msaidizi wake Kimani Kieya, msimamizi wa timu Joseph Kamau na kapteni Alex Mburu imeazimia kufukuzia taji katika mkundo wa pili kwani hatima yao nikuona timu inapaa ligini.

Isitoshe, wangependa kuendelea kustawisha talanta kauntini.

Kipa wa Kikosi cha Mutomo FC kutoka kaunti ya Gatundu Kusini akijipasaha moto kabla mechi kuanza.Picha/Patrick Kilavuka

Hata hivyo, wanasema ingawa timu inatoka kule viongozi watajika wanatoka, wangependa viongozi hao kushughulikia maslahi ya wanavipaji ili wapate jukwaa la kuvikuzia na kufanya vijana kutumia talanta zao vyema pamoja na kutumia wakati wao vyema pasi na kuzembea mitaani.

Isitoshe, waepukane na matumizi ya mihadarati kwa sababu maisha ya vijana yanaweza kuimarishwa tu na maadili kukuzwa kupitia michezo.

Kikosi ambacho kimebebe mwenge wa timu kauntini kufukuzia ligi ni Kipa Mike Owen, Alexander Mburu, Mathew Muchucha, Daniel Nguge, James Muronyo, Moses Kihara, Gidraff Thuo, Kevin Ndirangu, Seeid Ndichu, John Ndichu na David Karanja.

Wengine ni Joseph Wainaina, Joseph Muchiri, John Githongo, David Gitata, Christopher Kimemia Lukus Mburu na kadhalika.