• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Mwanariadha Wilson Kipsang taabani baada ya kupigwa marufuku ya miaka minne

Mwanariadha Wilson Kipsang taabani baada ya kupigwa marufuku ya miaka minne

Na CHRIS ADUNGO

MSHIKILIZI wa zamani wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Wilson Kipsang, 38, amepigwa marufuku ya miaka minne na Shirikisho la Riadha Duniani kwa msururu wa makosa ya kukiuka kanuni zinazodhibiti matumizi ya pufya.

Kati ya makosa yaliyochangia adhabu hiyo kali kwa mwanariadha huyo, ni tukio la Kipsang kuwasilisha picha ghushi ya ajali ya barabarani ili kutetea hatua yake ya kukosa kujiwasilisha kwa vipimo vya afya ili kubaini iwapo aliwahi kushiriki matumizi ya dawa haramu za kusisimua misuli au la.

Kitengo cha Maadili cha IAAF (AIU) kinadai kwamba Kipsang ambaye pia ni mshindi wa medali ya shaba katika Olimpiki za 2012, alikosa kujiwasilisha mara nne kwa vipimo hivyo vya afya kati ya Sprili 2018 na Mei 2019.

Kwa mujibu wa kanuni, mwanariadha anayekosa kujiwasilisha kwa minajili ya vipimo mara tatu chini ya kipindi cha miezi 12 hupigwa marufuku moja kwa moja.

Japo kikawaida makosa ya Kipsang yangalimpa adhabu ya kupigwa marufuku kwa mwaka mmoja pekee, ukali wa adhabu yake ulichangiwa na hatia ya kujaribu kuvuruga uchunguzi kwa kuwasilisha “ushahidi usio sahihi katika juhudi za kujitetea,”

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 38 ambaye ni mshindi mara mbili wa mbio za London Marathon, anajivunia rekodi ya saa 2:03:13 katika marathon ya dunia, muda ambao ni wa sita bora zaidi katika historia ya mbio za kilomita 42.

Katika kujitetea kwake, Kipsang alisema kwamba alikosa kujiwasilisha kwa vipimo vya afya mnamo Mei 2019 baada ya kupata ajali iliyohusisha lori lililopinduka barabarani.

Ingawa hivyo, ilibainika kwamba picha aliyowasilisha kuthibitisha madai hayo ilikuwa ya ajali iliyotokea Agosti 2019, miezi mitatu kutoka kwa muda aliodai Kipsang.

Mwaka mmoja baadaye, Kipsang alidai kwamba maporomoko ya ardhi kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikishuhudiwa nchini Kenya ilimzuia kufanyiwa vipimo vingine vya afya. Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kwamba hakukuwa na ithibati kwamba hali ya hewa ilikuwa mbaya humu nchini katika kipindi hicho kilichodaiwa na mwanariadha huyo.

Ikitangaza adhabu hiyo kwa Kipsang, vinara wa AIU walisema: “Kipsang alihusika katika udanganyifu jinsi ilivyobainishwa na miendendo yake. Hatua yake ya kuwasilisha ushahidi wa uongo ilipania kuzuia au kuvuruga taratibu za kawaida za IAAF katika vita vya kukabiliana na matumizi ya pufya.”

Volare Sports ambao ni wasimamizi wa Kipsang wamefichua mpango wa kukata rufaa dhidi ya marufuku ya AIU.

“Hakuna tukio lolote la matumizi ya pufya lililowahi kuripotiwa dhidi ya Kipsang. Tutathmini upya mchakato uliochangia kutolewa kwa adhabu hiyo kabla ya kuona hatua ya kuchukua. Tukisubiri hayo, hakuna lolote tunaloweza kusema kuhusiana na marufuku ya IAAF.”

  • Tags

You can share this post!

Messi achoshwa na Barcelona

CORONA:  Hali si hali baadhi ya wakazi wa mijini wakihamia...

adminleo