• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Mwanasoka atia saini kucheza hadi umri wa miaka 53

Mwanasoka atia saini kucheza hadi umri wa miaka 53

Na GEOFFREY ANENE

MSAKATAJI mzee wa kabumbu duniani Kazuyoshi Miura amesaini kandarasi mpya itakayoshuhudia akiendelea kuvalia daluga zake hadi atakapofikisha umri wa miaka 53.

Miura ni mshambuliaji wa kati kutoka Japan ambaye alizaliwa Februari 26 mwaka 1967 mjini Shizuoka.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti Januari 13, 2020 kuwa Miura, ambaye amekuwa akisakata soka kwa miaka 34, amesaini kandarasi ya mwaka mmoja na Yokohama FC.

Klabu ya Yokohama itashiriki Ligi Kuu nchini Japan mwaka 2020 baada ya kupata tiketi kwa kumaliza Ligi ya Daraja ya Pili katika nafasi ya pili nyuma ya Kashiwa Reysol anayochezea Mkenya Michael Olunga mwaka 2019.

Miura, ambaye jina lake la utani ni King Kazu, alichezeshwa mara tatu pekee ligini msimu uliopita ikiwemo katika mechi ya Yokohama ya kufunga msimu dhidi ya Ehime FC alipoingizwa katika nafasi ya Yusuke Matsuo, 22, dakika ya 87.

Dakika tatu alizopewa katika mechi hiyo zilidhaniwa kama mechi yake ya kuwapa mashabiki kwaheri, lakini sasa atakuwa kikosini Ligi Kuu ya Japan itakapoanza mwezi ujao wa Februari.

Miura, ambaye amekuwa akichezea Yokohama tangu mwaka 2005, amenukuliwa na tovuti ya klabu hiyo akisema, “Katika msimu wa 2020, nilifaulu kuongeza kandarasi yangu na Yokohama FC. Timu hii itakapoanza kampeni yake ya Ligi Kuu, nitajitahidi kabisa kuisaidia kusalia katika Ligi Kuu. Natumai kufurahia kuendelea kucheza soka na kukumbuka kutoa shukrani ninapoweka bidii kutimizia klabu malengo yake ya kusalia Ligi Kuu. Nitajikaza kisabuni kuchangia katika timu hii kushinda mechi.”

Miura alianza kutandaza soka mwaka 1982 akivalia jezi ya Juventus nchini Brazil na pia kuchezea Santos, Matsubara-PR, Regatas, Piracicaba, Coritiba nchini humo kabla ya kurejea Japan mwaka 1990.

Kisha, Miura alielekea Bara Ulaya mwaka 1994 kuchezea Genoa nchini Italia akarejea nchini mwake mwaka mmoja baadaye kabla ya kujiunga na Dinamo Zagreb nchini Croatia mnamo Januari 1, 1999. Alirejea nyumbani Japan mwezi Julai 1999 na kuchezea klabu kadhaa ikiwemo Yokohama kabla ya kutua Sydney FC nchini Australia kwa mkopo Oktoba 2005 na kisha kurejea Yokohama mwezi Desemba 2005.

Alichezea timu ya taifa ya Japan mara 89 kati ya mwaka 1990 na 2000 akiifungia mabao 55.

You can share this post!

City Stars yazidi kutetemesha BNSL

Wataka kampuni ya mawe ifungwe

adminleo