Nairobi Stima yatamba NSL
Na JOHN KIMWERE
FREDRICK Kentile aliangusha kombora moja safi kunako dakika ya tisini na kusaidia Ushuru FC kujizolea pointi moja kwenye mechi ya Supa Ligi ya Taifa (NSL) baada ya kutoka sare ya goli 1-1 na Administration Police (AP) uwanjani Ruaraka, Nairobi.
Nayo Nairobi Stima ilichoma Maafande wa APs Bomet kwa magoli 3-2 na kuendelea kukaa kileleni mwa jedwali kwa kusajili alama tisa sawa na Bidco United tofauti ikiwa idadi ya mabao. AP ililazimishwa kutoka nguvu sawa licha ya Humphrey Alemba kuiweka kifua mbele dakika ya 76.
Matokeo hayo yamefanya Ushuru FC ya kocha, James ‘Odijo’ Omondi kushuka hadi nafasi ya nne bora kwa kuvuna alama saba, sawa na Nairobi City Stars inayofunga tatu bora kutokana na idadi ya mabao.
Baada ya Ushuru FC kushinda mechi ya ufunguzi kocha huyo alisema ”Tunafahamu mambo siyo mteremko lakini tumepania kukazana kwa udi na uvumba ili kutwaa tikiti ya kusonga mbele msimu ujao.”
Naye Emmanuel Mogaka alitikisa nyavu mara moja na kubeba Bidco United kuzaba FC Talanta bao 1-0, Kenya Police ilibanwa 1-0 na Fortune Sacco huku Mt Kenya ikichapa Northern Wanderers 2-1.
St Josephs Youth ililima Kibera Black Stars 2-1, Migori Youth ilizoa 2-1 mbele ya Coast Stima, Shabana FC ililaza Modern Coast Rangers 3-2, nazo Murang’a Seal na Vihiga United kila moja iliagana sare tasa dhidi ya Vihiga Bullets na Nairobi City Stars mtawalia.