Naishukuru Gor kwa kuniondolea balaa – Owusu
BY CECIL ODONGO
KIUNGO wa Gor Mahia raia wa Ghana Jackson Owusu amefichua kwamba anaendelea vyema, wiki chache tu baada ya kuzuiliwa kwenye hoteli ya Jimlizer, Buruburu baada ya K’Ogalo kukosa kulipa bili ya Sh600,000
Owusu ambaye bado anaishi kwenye hoteli hiyo alieleza Taifa Leo kwamba masuala yote yaliyozua utata yalisuluhishwa na uongozi wa Gor. Aliongeza kwamba kwa sasa anaendelea kuhudumiwa vyema na usimamizi wa hoteli ya Jimlizer.
Mwanadimba huyo alikosa kusafiri hadi Ghana kabla ya janga la corona kutua hapa nchini.
Wachezaji wengine wa kigeni wa Gor Mahia David Mapigano na Dickson Ambudo wote raia wa Tanzania na mshambulizi wa K’Ogalo raia wa Uganda Juma Balinya, walifaulu kurejea katika mataifa yao kabla ya serikali kufutilia mbali safari za ndege nje na ndani ya nchi kama njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo vya maangamizi.
“Kwa sasa naendelea vizuri na maisha yangu hapa Kenya. Ningependa kushukuru uongozi wa Gor Mahia hasa Mwenyekiti Ambrose Rachier kwa kuyashughulikia masuala ambayo yalinifanya niteseke hapo awali,” akasema Owusu kwenye mahojiano na Taifa Leo
“Pia nawashukuru wafuasi wa Gor Mahia ambao walinisaidia wakati mgumu wa shida. Kwa sasa mambo yanaendelea vyema na hata familia yangu huko Ghana wanaishi kwa amani,” akaongeza.
Mwanadimba huyo alisema bado anafuatilia kwa karibu jinsi janga la corona limeathiri watu wa taifa lake na dunia nzima.
Ili kuhakikisha anaendelea kuwa fiti, mwanasoka huyo hufanya mazoezi kivyake nyakati za jioni katika uwanja moja wa umma karibu na kituo cha polisi cha Buruburu.
“Shughuli za michezo bado hazijarejelewa hata Ghana. Hata hivyo, mchezaji lazima awe fiti ndiyo maana sikosi kufanya mazoezi kila jioni,” akaongeza.
Owusu pia alihakikishia mashabiki wa Gor Mahia kwamba ataendelea kuchezea timu hiyo msimu ujao na hata kuisaidia kung’aa kwenye kipute cha Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF).
Kiungo huyo alijiunga na Gor Mahia wakati wa dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji mnamo Januari 2020.
Amekuwa mwanasoka tegemeo kwa mabingwa hao mara 18 wa Ligi Kuu ( KPL) chini ya ukufunzi wa kocha Steve Polack.
Kiungo huyo mvamizi pia alifanya kazi pamoja na Polack alipokuwa akichezea Asante Kotoko ya Ghana mnamo 2018.