Michezo

Napoli watwaa Coppa Italia

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NAPOLI waliwazidi Juventus maarifa kwenye fainali ya Coppa Italia ambapo mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti na kujinyakulia taji lao la kwanza baada ya kipindi cha misimu sita.   

Napoli waliwapiku washindani wao hao wakuu katika soka ya Italia kwa mabao 4-2 baada ya kuambulia sare tasa mwishoni mwa muda wa kawaida wa dakika 90 uwanjani Olimpico.

Arkadiusz Milik aliwafungia Napoli penalti ya ushindi baada ya Paulo Dybala kushuhudia mkwaju wake wa kwanza kwa upande wa Juventus ukipanguliwa na kipa Alex Meret kisha ule uliochanjwa na Danilo ukipaa juu ya mwamba wa goli la Napoli.

Ushindi wa Napoli ulimvunia Gennaro Gattuso taji lake la kwanza akiwa mkufunzi huku mwenzake Maurizio Sarri akisalia kusikitikia nafasi nyingi zilizopotezwa na vijana wake katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Sarri ambaye aliwahi kudhibiti mikoba ya Napoli kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhamia Chelsea anajivunia taji moja pekee la Europa League aliowanyanyulia miamba hao wa soka ya Uingereza kabla ya kurejea Italia kudhibiti mikoba ya Napoli mwishoni mwa msimu uliopita.

Japo wanaselelea kwa sasa kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa alama 63, ni pengo la pointi moja pekee ndilo linalotamalaki kati ya Juventus na Lazio ambao wanapigiwa upatu wa kuwapiku katika kampeni za muhula huu.

Penalti nyinginezo za Napoli zilifumwa wavuni na Lorenzo Insigne, Matteo Politano na Maksimovic.

Katika enzi yake ya usogora, Gattuso aliwaongoza Italia kujinyanyulia ubingwa wa Kombe la Dunia kabla ya kujizolea pia mataji ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Serie A akivalia jezi za AC Milan.

Mara ya kwanza kwa Gattuso kukaribia kujinasia taji akiwa kocha ni mnamo 2017 alipowaongoza AC Milan kutinga fainali ya Coppa Italia ila wakadenguliwa na Juventus kwa kichapo cha 4-0.

Gattuso aliaminiwa kudhibiti mikoba ya Napoli mnamo Disemba 2019 baada ya kuondoka kwa Carlo Ancelotti aliyeyoyomea Uingereza kuwatia makali vijana wa Everton. Mara ya mwisho kwa Napoli kujinyakulia ubingwa wa Coppa Italia ni 2014.

Kwa mujibu wa Gattuso, hamasa yao katika mechi dhidi ya Juventus ilichangiwa na ushindi wa Juni 14, 2020 ambapo waliwazamisha Inter Milan kwenye nusu-fainali ya Coppa Italia. Mchuano huo ulimpa mvamizi mzawa wa Ubelgiji, Dries Mertens jukwaa la kufunga bao lililomfanya mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Napoli.

Napoli kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kwenye jedwali la Serie A huku pengo la alama 24 likitamalaki kati yao na viongozi wa jedwali, Juventus.