Michezo

Ndidi kukosa mechi za Leicester kwa wiki 12 kutokana na jeraha

September 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

KIUNGO wa Leicester City, Wilfred Ndidi, 23, atasalia nje kwa wiki 12 baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na jeraha la kinena alilolipata kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 20, 2020.

Nyota huyo mzawa wa Nigeria amekuwa akiwajibishwa na Leicester kama beki katika siku za hivi karibuni baada Jonny Evans kuugua.

“Ni jeraha baya. Yasikitisha kwamba tutamkosa Ndidi kwa miezi mitatu hivi baada ya kufanyiwa upasuaji. Kutokuwepo kwake kutatutikisa pakubwa,” akasema kocha Brendan Rodgers.

“Naamini atapona haraka jinsi tunavyotarajia na atarejea ugani kwa matao ya juu na kuendeleza matokeo bora ambayo amekuwa akijivunia,” akaongeza kocha huyo wa zamani wa Liverpool.

Ushindi wa 3-0 na 4-2 uliosajiliwa na Leicester dhidi ya West Bromwich Albion a Burnley mtawalia katika mechi mbili za ufungunzi wa msimu huu uliwakweza hadi kileleni mwa jedwali la EPL.

Kikosi hicho kinatarajia sasa kujinyanyua ligini dhidi ya Manchester City mnamo Septemba 27, 2020, baada ya kudenguliwa na Arsenal kwenye Carabao Cup muhula huu kwa kichapo cha 2-0 mnamo Septemba 23 ugani King Power.