Ndindi Nyoro: Sisi Man U tulikubali kichapo cha Arsenal wasianze kulialia
Na MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, amedai kwamba Manchester United ilipoteza kwa hiari mechi yake ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Arsenal mnamo Mei 12, 2024.
Katika mechi hiyo iliyochezewa ugani Old Trafford, bao la Leandro Trossard kunako dakika ya 20 liliiwezesha Arsenal kukaa ngumu katika uwaniaji wa taji la EPL msimu huu wa 2023/24 uliobakisha juma moja uishe.
Arsenal inayoongoza jedwali kwa sasa, imecheza mechi 37 kati ya zote 38 na kuzoa pointi 86 huku Manchester City iliyo ya pili lakini baada ya kucheza mechi 36.
“Sisi tuliamua kuwasaidia hawa Arsenal ili wasije kutulaumu wakikosa kutwaa ligi. Sisi hatukati waishi kwa majuto ya kusema tuliwaharibia msimu,” akasema Bw Nyoro.
Alisema kwamba Arsenal ilihitaji kuhurumiwa.
“Arsenal inalia kuhusu Aston Villa na ndipo tukaagana kwamba tuwapishe wakaangukie mbele,” akatania mbunge huyo.
Bw Nyoro alisema kwamba ni juu ya Arsenal sasa “iongee vizuri na timu za Tottenham Hotspur na West Ham United ambazo ziko na udhia wa kumaliza na Man City ili nao waisaidie kama tulivyofanya”.
Alisema yeye anaitakia Man City na Arsenal mazuri katika ligi na ndiyo sababu “naomba kila mojawapo ya timu hizo wao ishinde mechi zake ilizosalia nazo”.
Iwapo kila mojawapo ya timu hizi mbili itashinda mechi zilizosalia, basi Man City itaibuka bingwa kwa pointi 91 huku nayo Arsenal ikibakia ya pili kwa pointi 89.