• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ndondi: Friza apoteza kushiriki Olimpiki, Kenya Ikirudi mikono mitupu

Ndondi: Friza apoteza kushiriki Olimpiki, Kenya Ikirudi mikono mitupu

NA CHARLES ONGADI

MATUMAINI ya mabondia wa Kenya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki katika Mashindano ya Dunia nchini Italia yaliyoyomea kama moshi baada ya Friza Anyango Asiko kushindwa mnamo Jumamosi, Machi 9, 2024.

Friza anayechezea klabu ya Majeshi (KDF) katika mashindano ya ligi kuu nchini, alishindwa na Walsh Grainne wa Irish katika pigano la raundi ya 16 uzani wa Welter.

Katika pigano hilo, Friza alionesha ukakamavu ulingoni akipigana kwa ujasiri mkubwa kuanzia mwanzo wa mchezo hadi tamati.

Kabla ya kutinga hatua ya 16 bora, Friza alimkung’uta Chiroy Maria wa Guatemala kwa pointi 4-1 na kuwa bondia wa pekee wa Kenya kuandikisha ushindi katika mashindano hayo.

Bondia Shaffi Bakari pia wa Kenya alishindwa kwa wingi wa alama na Rustamov Umid wa Azerbaijan katika pigano la uzani wa unyoya.

Hata licha ya kupoteza pigano hilo, wadau wengi wa mchezo wa masumbwi nchini walimpongeza sana bondia huyu kwa ujasiri alioonyesha katika mashindano hayo.

Mwamba wa zamani wa timu ya taifa Ibrahim ‘Surf’ Bilali ni baadhi ya wapenzi wa masumbwi nchini waliokuwa mstari wa mbele kumpongeza Friza kwa ustadi alioonyesha katika mashindano hayo.

Licha ya mabondia wa Kenya kushindwa kufuzu katika mashindano haya ya Italia, wangali na nafasi ya mwisho kusaka tikiti ya kushiriki Michezo ya Olympiki yatakayoandaliwa jijini Paris nchini Ufaransa kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8.

Mashindano ya pili ya dunia kusaka nafasi ya kufuzu yameratibiwa kuandaliwa Bankok nchini Thailand, kuanzia Mei 26 hadi June 2.

Mabondia wengine waliowakilisha taifa katika mashindano haya ya dunia ni Christine Ongare (Fly), David Karanja (Fly), Shaffi Bakari (Unyoya), Boniface Mogunde (Light middle) na Elizabeth Andiego (Middle).

Kwingineko, kocha John Waweru ameiambia Taifa Spoti kwamba ana uhakika mabondia wanne watakaowakilisha taifa katika mashindano ya Afrika jijini Accra nchini Ghana watafanya vyema.

“Mabondia wote wanne wana uwezo wa kurudi nyumbani na medali za dhahabu hasa kutokana na mazoezi tuliyoshiriki na fomu yao katika mashindano ya kitaifa nchini,” akasema kocha Waweru.

Mabondia watakaopeperusha bendera ya taifa nchini Ghana ni Amina Faki Martha katika uzani wa Bantam, Alloyce Vincent (Light welter), Edwin Okong’o (Middle) na Peter Abuti (Heavy).

  • Tags

You can share this post!

Wamalwa akataaa marupurupu ya Nadco

Waislamu watakiwa kusubiri tangazo la Kadhi Mkuu kuhusu...

T L