Michezo

Ndoto ya Wanyama yazimwa

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

MATUMAINI ya kiungo Victor Wanyama kushiriki Klabu Bingwa ya Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) yalizimwa Alhamisi baada ya Montreal Impact kupoteza 3-1 dhidi ya Vancouver Whitecaps.

Nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya alichangia kwa pamoja na kiungo wa Algeria Saphir Taider pasi iliyosaidia Montreal kupata bao la kufuta machozi kutoka kwa mshambuliaji wa Honduras Romell Quioto dakika ya 70.

Vijana wa kocha Thierry Henry, ambao walikuwa ugenini Whitecaps, walijipata chini bao moja dakika ya 41 baada ya beki Mfaransa Rudy Camacho kusababisha penalti iliyofungwa na mshambuliaji Fredy Montero.

Camacho alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kupiga ngumi Montero ndani ya kisanduku cha Montreal. Montero alikuwa amemchezea visivyo, lakini refa Drew Fischer hakuwa ameadhibu mshambuliaji huyo kutoka Colombia.

Kiungo wa Colombia Cristian Dajome aliongeza bao la pili sekunde chache kabla ya mapumziko. Quioto alirejesha goli moja dakika ya 70, lakini matumaini ya Montreal kufufuka yalizimwa kabisa dakika nane baadaye Montero alipomwaga kipa kutoka Senegal Clement Diop.

Montreal iliingia mchuano huo ikishikilia nafasi ya pili kwenye mashindano ya Canada kwa alama tisa baada ya kusakata michuano mitano. Ilihitaji ushindi ili ing’oe Toronto FC kutoka kileleni. Iliingia mechi hiyo na motisha tele baada ya kupepeta Whitecaps mara mbili; 2-0 Agosti 26 na 4-2 mnamo Septemba 14. Toronto inasalia juu kwa alama 12 baada ya kupiga mechi zake sita. Whitecaps imekamilisha kampeni yake kwa alama sita baada pia kushinda Toronto 3-2 mnamo Septemba 6.

Mechi ya kwanza ya Wanyama baada ya kujiunga na Montreal akitokea Tottenham Hotspur nchini Uingereza ilikuwa kwenye Klabu Bingwa ya Concacaf dhidi ya Olimpia kutoka Honduras mnamo Machi 11. Montreal ililemewa 2-1 katika mechi hiyo ya robo-fainali.

TAFSIRI NA GEOFFREY ANENE