Michezo

Neymar aandamwa na mamlaka ya ushuru Uhispania alipe Sh4.4 bilioni

October 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

BARCELONA, Uhispania:

Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Neymar da Silva Santos Junior almaarufu Neymar ana deni la Sh4.4 bilioni la mamlaka ya kutoza ushuru nchini Uhispania.

Tovuti ya Get French News imesema Jumatano kuwa mamlaka hiyo imetoa orodha ya watu binafsi na kampuni inazowadai fedha.

“Katika orodha hiyo, kuna mshambuliaji wa Brazil na PSG, Neymar, ambaye anafaa kulipa ushuru wa Sh4.4 bilioni (Yuro 34.6 milioni),” tovuti hiyo imesema.

Kiasi hicho cha fedha, tovuti hiyo imefichua, kinatoshana na ushuru ambao Neymar hajalipa unaotokana na marupurupu aliyopokea kutoka kwa waajiri wake wa zamani Barcelona alipokuwa ameongeza kandarasi yake uwanjani Camp Nou mwaka 2016 kabla ahamie mjini Paris nchini Ufaransa mwaka 2017 akiwa hajakamilisha kandarasi yake.

Neymar alijiunga na PSG baada ya mawakili wake kulipa Barcelona Sh28.2 bilioni mnamo Agosti 3, 2017. Kiasi hicho kilikuwa ada ya kumruhusu aondoke Barca iliyokuwa imeweka kipengee cha kumzuia kuondoka kabla ya kiasi hicho kutolewa katika kandarasi yake.

Uhamisho wa Neymar kutoka Barca hadi PSG unasalia kuwa ghali kuwahi kushuhudiwa katika historia ya soka. Barca ilishtaki Neymar hapo Agosti 27 mwaka 2017 ikitaka arejeshe marupurupu ya kusaini kandarasi mpya uwanjani Camp Nou, fidia ya Sh1.08 bilioni pamoja na nyongeza ya asilimia 10 ya malimbikizi.

Mwaka 2016, mahakama moja jijini Rio de Janeiro nchini Brazil pia ilipata Neymar na hatia ya kulaghai mamlaka ya ushuru nchini mwake ili kujinufaisha. Alitozwa faini ya Sh5.8 bilioni, ambayo ilikuwa ushuru, faida na faini. Inasemekana wakati huo Neymar alikuwa amekwepa kulipia ushuru mapato yake kwenye kandarasi zake kati ya mwaka 2011 na 2013 ambazo zilikuwa kutoka klabu yake ya zamani Santos nchini Brazil, Barcelona pamoja na kampuni ya vifaa vya michezo, Nike. – Imetafsiriwa na Geoffrey Anene