• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:09 PM
Neymar afunga penalti dhidi ya RB Leipzig na kumpunguzia presha kocha Tuchel

Neymar afunga penalti dhidi ya RB Leipzig na kumpunguzia presha kocha Tuchel

Na MASHIRIKA

PENALTI ya kipindi cha kwanza iliyofungwa na Neymar Jr ilimpunguzia kocha Thomas Tuchel presha ya kufutwa kazi na Paris Saint-Germain (PSG) waliowaruka RB Leipzig ya Ujerumani kwenye msimamo wa Kundi H baada ya ushindi wa 1-0 katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 24, 2020.

Neymar alifunga bao lake la kwanza baada ya mechi sita baada ya fowadi Angel di Maria kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku katika dakika ya 11.

Ingawa wanasoka wa Julian Nagelsmann walijitahidi kurejea mchezoni, walipoteza nafasi nyingi za wazi katika mchuano huo uliotandaziwa ugani Parc des Princes, Ufaransa. Dayot Upamecano, Emil Forsberg na Marcel Sabitzer ni miongoni mwa wanasoka waliopoteza nafasi hizo licha ya kusalia uso kwa macho na kipa wa PSG.

Leipzig kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kundini kwa alama sita sawa na PSG wanaowazidi kwa wingi wa mabao. Manchester United wanaselelea kileleni kwa alama tisa huku zikisalia mechi mbili zaidi kwa kampeni za makundi kutamatika.

Istanbul Basaksehir kutoka Uturuki watakuwa wenyeji wa Leipzig katika mchuano wao ujao ambao wana ulazima wa kushinda ili kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa hatua ya mwondoano.

Matokeo kati ya PSG na Leipzig yalirejesha kumbukumbu za msimu wa 2019-20 ambao ulishuhudia PSG wakibandua kikosi hicho cha Ujerumani katika hatua ya nusu-fainali.

Mbali na Neymar aliyekuwa mfungaji wa bao la pekee na la ushindi, mchezaji mwingine aliyeridhisha zaidi kambini mwa PSG ni kiungo raia wa Italia, Marco Verratti aliyekuwa akirejea kikosini baada ya jeraha kumweka nje kwa zaidi ya wiki sita zilizopita.

Chini ya Tuchel, PSG kwa sasa wanajiandaa kurudiana na Man-United katika mchuano wao ujao wa UEFA ugani Old Trafford mnamo Disemba 2, 2020.

Watapania kulipiza kisasi katika gozi hilo baada ya vijana wa mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer kuzamisha chombo chao kwa mabao 2-1 mnamo Oktoba 20, 2020, nchini Ufaransa.

You can share this post!

Haaland abeba Dortmund na kuweka historia ya ufungaji...

Uchomaji makaa Boni ungali tishio kwa uhifadhi wa mazingira