Michezo

Neymar asema atatua Real ikimlipa Sh165m kwa juma

May 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

FOWADI mzaliwa wa Brazil Neymar Jr, 27, amewataka Real Madrid kumpa hakikisho kwamba watamlipa mshahara wa hadi Sh165 milioni kwa wiki iwapo atajiunga nao uwanjani Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa gazeti la AS nchini Uhispania, Neymar atakuwa radhi kuagana na Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa kufikia Julai iwapo Real ambao wangali wanapania kulijaza pengo la Cristiano Ronaldo, watatimiza masharti hayo.

Ili kufanikisha mpango huo, huenda kocha Zinedine Zidane akalazimika kumtia mshambuliaji mzaliwa wa Wales, Gareth Bale mnadani ili kupunguza gharama ya kumdumisha Neymar kimshahara.

Kufikia sasa, Neymar hutia mfukoni kima cha Sh85 milioni kwa wiki kambini mwa PSG ambao walifaulu kumng’oa katika kikosi cha Barcelona kwa Sh26 bilioni mnamo 2017.

Fedha hizo zilizowekwa mezani na PSG kwa minajili ya huduma za Neymar, zilimfanya fowadi huyo akiweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi duniani.

Tangu Ronaldo arasimishe uhamisho wake hadi kambini mwa Juventus nchini Italia mwishoni mwa msimu jana, Bale kwa sasa ndiye mchezaji anayepokezwa mshahara wa juu zaidi katika kikosi cha Real.

Bale mwenye umri wa miaka 29 amekuwa na msimu mbaya zaidi muhula huu baada ya kushindwa kushirikiana vilivyo na Karim Benzema kulijaza pengo la Ronaldo.

Wepesi wake wa kupata majeraha ya mara kwa mara na kushuka pakubwa kwa ubora wa kiwango cha mchezo wake ni jambo ambalo huenda likawachochea Real kumuuza.

Ingawa azma yake ni kusalia uwanjani Bernabeu na kuwathibitishia wakosoaji wake vinginevyo, huenda usimamizi wa Real ukamshinikiza Zidane kumtema.

Mbali na kuzihemea huduma za Neymar, Real wanayawania pia maarifa ya chipukizi Kylian Mbappe wa PSG.

Baada ya kutawazwa Mchezaji Bora wa PSG msimu huu, Mbappe mwenye umri wa miaka 20 aliashiria kwamba huenda akawa radhi kubanduka kambini mwa waajiri wake na kuyoyomea Real iwapo watafungulia mifereji yao ya pesa na kuweka mezani kiasi cha Sh33 bilioni.

“Hiki ni kipindi muhimu sana kwangu. Ni wakati wa kutathmini upya mustakabali wa taaluma yangu katika ulingo wa soka. Nimebaini mengi mno ndani ya PSG na kwa sasa nahisi ni wakati wa kupokezwa majukumu makubwa ba mazito zaidi ama hapa PSG au kwingineko,” akasema Mbappe.

Hata hivyo, PSG wamefutilia mbali tetesi zote zinazomhusisha Mbappe na uwezekano wa kubanduka kambini mwao hivi karibuni.

Neymar na Mbappe wamewahi kujitokeza peupe na kukashifu mbinu za ukufunzi wa Thomas Tuchel aliyerefusha mkataba wake kambini mwa miamba hao wa soka ya Ufaransa hadi Juni 30, 2021.

Mkufunzi huyo mzawa wa Ujerumani alipokezwa mikoba ya PSG mnamo Juni 2018 na akawachochea waajiri wake kutia kapuni ufalme wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Hata hivyo, PSG ambao wanajivunia ukiritimba katika soka ya Ufaransa, walikabiliwa na wakati mgumu katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) huku wakidenguliwa na Manchester United kwenye hatua ya 16-bora.

French Cup

Isitoshe, walipepetwa na Rennes kwenye fainali ya French Cup baada ya kuzidiwa maarifa kupitia mikwaju ya penalti.

Tuchel amekiri kwamba mtihani mgumu zaidi alionao kwa sasa ni jinsi ya kuwadumisha kikosini Mbappe na Neymar ambao wanahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Real. Mvamizi wake mwingine wa haiba kubwa, Edinson Cavani amedokeza azma ya kustaafu katika timu ya taifa ya Uruguay baada ya mkataba wake na PSG kumalizika mwishoni mwa msimu ujao.

Wanapojiandaa kujaza pengo la Cavani, vinara wa PSG wameamua kumhemea Edin Dzeko wa AS Roma ambaye huenda akatua ugani Parc des Princes kufikia Julai mwaka huu.