Ni kifo kwa wapenzi wa pufya Bahrain
Na Geoffrey Anene
NCHI ya Bahrain, ambayo wanariadha kutoka Bara Afrika ikiwemo Kenya wamekuwa wakikimbilia kubadili uraia ili kuimarisha maisha yao kupitia ukumbiaji, inawazia kutunga sheria za kuhukumu watumiaji wa dawa za kusisimua misuli kifo.
Miezi michache baada ya Kitengo cha Maadili cha Riadha (AIU) kutangaza kinachunguza kesi 120 za matumizi ya pufya bingwa wa Olimpiki wa mita 3,000 kuruka maji na viunzi Ruth Jebet akiwa mmoja wao, Bahrain imesema inalenga kufanya adhabu ya uovu huu kuwa kali kabisa.
“Matumizi ya pufya ni suala la jamii nzima na jamii inafaa kuchukua msimamo,” Mwenyekiti wa Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini Bahrain, Dkt Khalid Al Shaikh amenukuliwa na tovuti ya GDN akisema Septemba 10, 2018.
“Tatizo hili ni kubwa na hatua tunayotaka kuchukua ni kutunga sheria zinazoharamisha matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwa sababu wakati huu hakuna adhabu kali isipokuwa kupokonya wanariadha medali na kuwapiga marufuku.
“Hatutaki tu kupiga dawa hizi marufuku; tunataka kuzichukulia kama dawa za kulevya kwa kufanya adhabu yake kuwa kifungo cha jela na hata wakati mwingine, hukumu ya kifo.”
Afisa huyo ameelezea madhara ya matumizi ya dawa hizi kwa kutoa mfano wa kijana mmoja mwa miaka 19, ambaye alidungwa sindano kupewa homoni ya kufanywa mwanaspoti matata. “Kijana huyo aliishia kupooza. Ni miaka minne sasa na hajapona; hawezi kutumia mikono yake wala miguu yake,” afisa huyo amesema.
Baadhi ya Wakenya ambao wamebadili uraia na kuwa Wabahraini ni Jebet, mshindi wa medali ya shaba ya Olimpiki ya mbio za marathon Eunice Kirwa pamoja na John Koech na Nelson Cherutich (mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Benson Kiplagat Seurei (mita 1500), Abraham Rotich (mita 800), Albert Rop (mita 5,000), Rose Chelimo, Isaac Korir na Abraham Cheroben (mita 10,000) na wengineo.
Bahrain imekuwa ikitafuta talanta za riadha kutoka Bara Afrika. Majuzi tu, Bahrain ilichemkiwa katika michezo ya Bara Asia iliposhinda medali 12, kumi zikipatikana kupitia kwa wakimbiaji kutoka Ethiopia, Nigeria, Kenya na Morocco.