Michezo

NI KIJASHO: Arsenal wageni wa Sheffield United

October 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Chris Wilder wa Sheffield United anatarajiwa leo Jumatatu kuwawajibisha masogora John Fleck, Oli McBurnie na David McGoldrick dhidi ya Arsenal watakaokuwa wageni wao uwanjani Bramall Lane, Uingereza.

Watatu hao walilazimika kujiondoa katika timu zao za taifa wiki iliyopita kutokana na majeraha mbalimbali. Kwa upande wao, Arsenal huenda wakamkaribisha mvamizi matata Alexandre Lacazette ambaye amekuwa mkekani kuuguza jeraha la kifundo cha mguu tangu mwanzoni mwa Septemba 2019.

Chipukizi Reiss Nelson ambaye kwa sasa anauguza jeraha la goti atasalia nje ya kikosi cha Arsenal hadi mwishoni mwa Novemba mwaka huu. Akiwataka vijana wake kujituma maradufu, Wilder anahisi kwamba kikubwa zaidi kitakachowatambisha dhidi ya Arsenal ni hamasa iliyowatawala dhidi ya Liverpool katika mchuano wao uliopita.

Japo Liverpool walisajili ushindi katika mechi hiyo, Sheffield walitamba vilivyo na kuonekana kuwazidi nguvu wapinzani wao katika takriban kila idara. Kiwango cha kujiamini kwa Sheffiled katika kivumbi hicho ni jambo ambalo Wilder anaamini kitawawezesha kuwakaba koo masogora wa kocha Unai Emery ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 15 jedwalini.

“Nadhani tulicheza vizuri zaidi dhidi ya Liverpool. Ingawa hakutujizolea alama tatu muhimu katika mchuano huo, mechi ya Jumatatu ni jukwaa bora zaidi la kujidhihirisha ukubwa wa uwezo tulionao. Sioni sababu yoyote itakayotunyima alama tatu muhimu dhidi ya Arsenal hasa ikizingatiwa kwamba tunacheza mbele ya mashabiki wetu wa nyumbani,” akasema kocha huyo.

Kufikia sasa, Sheffiled United wamejizolea alama sita ugenini na tatu pekee katika uwanja wao wa nyumbani wa Bramall Lane. Arsenal watashuka ugani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia alama tatu muhimu katika ushindi mwembamba wa 1-0 waliousajili dhidi ya Bournemouth katika mechi iliyopita.

Kati ya mechi 26 ambazo zimewahi kukutanisha vikosi hivi katika mashindano yote ya awali, Arsenal wanajivunia rekodi ya kupoteza mara tatu pekee. Ingawa hivyo, Sheffield almaarufu ‘Blades’ hawajapoteza mechi yoyote katika nne zilizopita dhidi ya Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) tangu Aprili 1991 walipotandikwa 2-0.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa Arsenal na Sheffield United kukutana ligini tangu 2006.

Kikubwa zaidi kinachofanya Arsenal kupigiwa upatu wa kusajili ushindi leo ni ushindi wa hivi karibuni wa mabao 9-0 waliousajili katika kivumbi cha League Cup.

Sheffield United wanajivunia kutofungwa bao tangu mwanzoni mwa msimu uliopita.

Ni kwa mara ya kwanza tangu 1972-73 ambapo Sheffield United hawajapoteza mechi yoyote kati ya nne zilizopita ugenini.

Itakuwa fursa yao ya kuzuia kushindwa katika jumla ya mechi nne mfululizo mbele ya mashabiki wa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu Aprili 1965.

Kwa upande wao, Arsenal hawajasajili ushindi wowote ugenini tangu wawazamishe Newcastle United katika mchuano wa ufunguzi wa msimu huu. Arsenal wanajivunia ufanisi wa kusajili ushindi mara saba katika mechi zote zilizopita uwanjani Bramall Lane. Kati ya mechi zote 11 za EPL ambazo wamewahi kuzisakata mnamo Jumatatu, Arsenal wamepoteza mchuano mmoja pekee uliowakutanisha na Crystal Palace mnamo Aprili 2017.