Ni kivumbi fainali za Chapa Dimba Kaskazini Mashariki
Na JOHN KIMWERE
USHINDANI mkali unatazamiwa kushushwa Jumanne kwenye nusu fainali kupigania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two Mkoani Kaskazini Mashariki zitakazopigiwa Ugani Garissa University.
Timu nne za wavulana zitaingia mzigoni kupigania ubingwa wa eneo hilo pia tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za kitaifa zitakazoandaliwa katika Uwanja wa Kinoru Stadium, Kaunti ya Meru mwezi Juni mwaka huu.
”Raundi huu tutaandaa fainali za Mkoa wa Saba kati ya nane kabla ya kumalizia Mkoani Nairobi wiki ijayo,” mshirikishi wa kipute hicho, Patrick Korir alisema.
Berlin FC ya Garissa imepangwa kukabili Dadaab United kutoka kambi ya Dadaab kwenye nusu fainali ya kwanza. Nayo Al Ansar FC kutoka Wajir itamenyana na timu kutoka Mandera kisha washindi watakutanishwa katika fainali Jumatano ya wiki hii.
Kando na tiketi ya kusonga mbele timu itakayoibuka bingwa wa eneo hilo itatuzwa kitita cha Sh200,000. Mshindi wa mkoa huo atajiunga na wenzao kutoka mikoa mingine ikiwamo:
Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa) bila kusahau Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati).
Mabingwa wa kitaifa timu ya wavulana pia wasichana kila moja itatuzwa kitita cha Sh 1 milioni.