NI KUBAYA: Kenya na Tanzania hatarini kufungishwa virago AFCON
Na GEOFFREY ANENE
TIMU za Kenya na Tanzania zilisalia kula makombo katika mechi zao za mwanzo Kundi C baada ya kuraruliwa na Algeria na Senegal kwa mabao 2-0 kila moja kwenye Kombe la Afrika (AFCON) jijini Cairo nchini Misri, Jumapili usiku.
Saa chache baada ya Tanzania ya kocha Emmanuel Amunike kuzamishwa na mabao ya Keita Balde na Krepin Diatta, Harambee Stars pia ilijipata pabaya ilipopokea dozi sawa na hiyo kupitia kwa Baghdad Bounedjah na nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez.
Vijana wa kocha Sebastien Migne, ambaye amekosolewa na mashabiki kwa kichapo hicho wakidai hakupanga kikosi chake vyema, ilikuwa na mchecheto katika kipindi cha kwanza.
Wakenya ambao hawakuwa wamefungwa bao katika dakika 45 za kwanza katika mechi saba zilizopita, walifunguwa mabao yote kabla ya mapumziko.
Beki Dennis Odhiambo, ambaye ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa katika timu ya Kenya (34), aliipa Desert Foxes ya Algeria fursa ya kupata kiamsha kinywa alipoangusha Youcef Atal ndani ya kisanduku akijaribu kuondosha hatari.
Bounedjah alimwaga kipa Patrick Matasi kupitia penalti iliyopatikana. Itakumbukwa kwamba Matasi aliingia katika mechi hii akiwa amepangua penalti mbili katika mechi za kirafiki Kenya ilipolima Barea ya Madagascar 1-0 Juni 7 jijini Paris nchini Ufaransa ilikokuwa na kambi ya mazoezi na kutoka 1-1 Juni 15 dhidi ya Leopards ya DR Congo jijini Madrid nchini Uhispania.
Mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2016 Mahrez alikuwa mwiba sana kwa Wakenya. Alipata fursa ya kuandikisha jina lake kwenye orodha ya wafungaji alipomegewa pasi safi kutoka kwa Sofiane Feghouli ndani ya kisanduku. Shuti yake iliguswa na Abud Omar na kuacha kipa bora wa Kenya mwaka 2016 na 2017 Matasi hoi.
Ayub Timbe na Eric Johanna walijaribu bahati dakika za mwisho mwisho za kipindi cha kwanza, lakini majaribio yao hayakulenga goli. Kenya iliimarika katika kipindi cha pili hasa baada ya Mfaransa Migne kumwingiza mechini Eric Ouma katika nafasi ya Francis Kahata.
Hata hivyo, mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) walikosa ujuzi wa kufunga bao. Mshambuliaji Michael Olunga, ambaye amekuwa akitegemewa sana kuchangia mabao, hakuwa na lake, huku Kenya ikisalimu amri baada ya kupoteza alama zote dhidi ya wafalme hao wa Afrika wa mwaka 1990.
Kenya, ambayo inarejea katika AFCON tangu mwaka 2004, ilimiliki mpira asilimia 40 pekee dhidi ya 60 ya Algeria. Vijana wa Migne walisababisha ikabu mara 28 ikiwemo Omar na Philemon Otieno kuonyeshwa kadi ya njano. Algeria iliadhibiwa mara 12 pekee.
Kabla ya Kenya kuonyeshwa kivumbi na Algeria, Tanzania ilikuwa imelazwa na Senegal katika mechi ya kwanza ya kundi hili. Vijana wa Amunike walikubali nyavu zao kutikiswa na Keita Balde dakika ya 28 na Krepin Diatta dakika ya 64.
Majirani Kenya na Tanzania watakutana katika mechi ijayo mnamo Juni 27, huku Algeria na Senegal zikimenyana katika mchuano mwingine siku hiyo, mechi ambayo ni kama fainali kabla ya fainali. Eneo la Cecafa pia lina Uganda iliyokanyaga DR Congo 2-0 katika mechi ya Kundi A na Burundi iliyopoteza 1-0 dhidi ya Nigeria katika mechi ya Kundi B.
Timu mbili za kwanza kutoka makundi yote saba zitaingia moja kwa moja katika raundi ya 16-bora.
Timu nne zitakazokamilisha mechi za makundi katika nafasi ya tatu zikiwa na alama nyingi pia zitafuzu kwa awamu hiyo.