• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
NI MTIMKO! Riadha za Dunia kutifua vumbi Doha

NI MTIMKO! Riadha za Dunia kutifua vumbi Doha

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa mwaka 2015 Kenya watakuwa mbioni kutafuta medali yao ya kwanza katika makala ya 17 ya Riadha za Dunia zitakazotifua vumbi leo Ijumaa jioni jijini Doha nchini Qatar.

Kenya huenda ikaanza mavuno yake ya medali usiku wa kuamkia Jumamosi wakati wakimbiaji Edna Kiplagat, Visiline Jepkesho na Ruth Chepng’etich watakaposhindania taji la mbio za kilomita 42.

Kiplagat anajivunia mataji ya mwaka 2011 (Korea Kusini) na 2013 (Urusi). Ana uzoefu mkubwa. Mbali na mataji hayo, Kiplagat alimaliza makala ya mwaka 2015 nchini Uchina katika nafasi ya tano kabla ya kujinyakula medali ya fedha miaka miwili iliyopita jijini London nchini Uingereza.

Mzawa wa Kenya, Rose Chelimo alishindia Bahrain taji jijini London akikata utepe kwa muwa saa 2:27:11, sekunde saba mbele ya Kiplagat na Mwamerika Amy Cragg aliyeandikisha muda sawa na Kiplagat.

Inamaanisha kuwa Kiplagat, ambaye alisherehekea umri wa miaka 40 tangu azaliwe, majuma mawili yaliyopita, atalazimika kufanya kazi ya ziada ili astaafu na medali nyingine.

Malkia huyu wa mbio za kifahari za kilomita 42 za New York (2010), London (2014) na Boston (2017) atashirikiana na Jepkesho, ambaye hakuridhisha katika jaribio lake la kwanza kwenye Riadha za Dunia mwaka 2015 alipomaliza katika nafasi ya 20.

Alisikitisha zaidi mwaka uliofuata katika Michezo ya Olimpiki alipokamilisha mbio hizo katika nafasi ya 86. Jepkesho, 29, ana uzoefu wa miaka mitano katika mbio hizi ndefu, kwa hivyo huenda akawa na kismati wakati huu.

Naye Chepng’etich amekuwa akipata ufanisi mkubwa katika mbio za kilomita 21. Alidhihirisha kuwa yuko fiti katika marathon aliponyakua taji la Dubai Marathon mapema mwaka huu kwa saa 2:17:08, sekunde saba pekee nje ya rekodi ya dunia inayoshikiliwa na Mkenya mwenzake Mary Keitany.

Ushindani mkali kwa Wakenya hao unatarajiwa kutoka kwa Mbahraini Chelimo, Mwisraeli Lonah Chemtai Salpeter, ambaye pia ni mzawa wa Kenya, Mtanzania Failuna Matanga pamoja na wakimbiaji kutoka Ethiopia, Japan na Namibia.

Mbali na marathon, Wakenya leo watakuwa mawindoni katika mbio za mita 800 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji (wanawake) na mbio za mita 5,000 na mita 400 kuruka viunzi (wanaume) kutafuta tiketi za kusonga mbele.

Mbio za mita 800

Eunice Sum atabeba matumaini yote ya Kenya kupata medali katika mita 800 za wanawake pekee yake.

Bingwa huyu wa dunia mwaka 2013 atakuwa akitafuta tiketi ya kuingia nusu-fainali leo Ijumaa.

Kenya ina wakimbiaji matata Celliphine Chespol, mshikilizi wa rekodi ya dunia Beatrice Chepkoech, Fancy Cherono na bingwa wa mwaka 2015 Hyvin Kiyeng katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Kibarua chao cha kwanza ni kufuzu kushiriki fainali. Chepkoech, ambaye amekuwa na msimu mzuri mwaka huu, alimaliza katika nafasi ya nne miaka miwili iliyopita wakati Kenya iliporidhika na shaba kupitia kwa Kiyeng.

Jacob Krop na Nicholas Kimeli watahitajika kufanya kazi ya ziada sio tu ya kufika fainali ya mbio za mita 5,000, bali kuondolea Kenya masikitiko ya kuambulia pakavu miaka miwili iliyopita.

Mataifa 208 yanashiriki makala haya. Timu ya wakimbizi pamoja na ile ya wakimbiaji kutoka Urusi waliodhinishwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) pia zinashiriki.

Taifa la Urusi lilipigwa marufu kutokana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwa hivyo haliwezi likawakilishwa moja kwa moja katika riadha hizi.

Ratiba ya leo Ijumaa

Mchujo wa 800m (wanawake, 5.10pm); Mchujo wa 3,000m kuruka viunzi na maji (wanawake, 6.55pm); Mchujo wa 5,000m (wanaume, 7.45pm); Fainali ya marathon (wanawake, 11.59pm).

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Gatundu wahakikishiwa usalama wao

CARABAO: Arsenal, Chelsea kulimana na Liverpool na...

adminleo