Nidhamu nguzo kuu ya Kiranga United FC
Na LAWRENCE ONGARO
TIMU ya soka ya Kiranga United FC ya Kaunti ya Murang’a, tayari imekoleza mizizi yake miaka mitano iliyopita huku dhamira yake ikiwa ni kuendelea kucheza mechi za mataji na za kirafiki.
Kocha chipukizi wa timu hiyo Samuel Nyoike, anasema kwa sasa wanashiriki ligi ya tarafa za wadi ambapo wanawania taji la Mbunge wa Kandara Bi Alice Wahome.
“Kwa sasa ninakuza kikosi cha vijana 22 huku tukiunda timu stadi yenye ujuzi tele,” anasema kocha Nyoike.
Anasema tayari ameunda kikosi kinachojumuisha vijana chipukizi kati ya miaka 17 na 24 huku wakiwa wamejitolea kusakata boli kwa bidii.
Aidha, kocha Nyoike anasema kiini cha klabu hiyo kupiga hatua tangu wakati huo wote ni kutokana na nidhamu huku kila mchezaji akijituma kwenda mazoezini bila kushurutishwa na yeyote.
Kocha huyu anasema anatamani kuona vijana wake wakiboresha mchezo wao na kufuzu kucheza soka ya kiwango cha juu.
“Nina imani kuwa kila mchezaji ana nafasi yake katika uchezaji wa soka na kwa hivyo ni vyema kujitahidi,” anasema.
Anasema kuwa kwa wakati huu vijana wake wako katika harakati ya kucheza ligi ya wadi ya Muruka huku timu 14 zikishiriki.
Miezi mitatu zilizopita pia walishiriki katika dimba la kuwania taji la James Ngugi Cup, ambapo waliweza kufika fainali na kuichabanga Kihumbu-ini mabao 2-1.
Anasema kikosi chake kinaendeshwa na maafisa waliojitolea mhanga kuona ya kwamba Kiranga United inapiga hatua katika kiwango kingine.
Mwenyekiti wake ni Julius Mungai Rung’u. Katibu ni David Mararo. Mweka hazina ni John Mburu. Halafu nahodha wa timu ni Harisson Ng’ethe.
Wachezaji wanaoipa uhai klabu hiyo ni kipa Simon Muiruri, difensi kuna Joseph Chege, Peter kariuki, Harisson Ng’ethe na Isaac Mugo. Kiungo kuna James Muturi, Edwin Mwaura, Anthony Kariuki, na John Kariuki. Mastraika ni James Wainaina, Gibon Kairu, Maina Charles na Anthony Ndung’u.
Hata hivyo anamsifu sana mlezi wa klabu hiyo Elijah Mwangi Kinuthia, ambaye kwa ukarimu wake ameweza kununua jezi za kuchezea pea sita na ni hivi majuzi aliponunulia kikosi kizima pea 11 za njumu (Viatu).
Anatoa mwito kwa wafanyi biashara hasa mabwanyenye ambao wanajiweza kifedha kuingilia kati na kuisaidia klabu hiyo.
Anasema atazidi kuwapa vijana wake motisha ili kupata mabadiliko katika uchezaji wao wa soka. Hayo yatafanikiwa tu iwapo watafuata maagizo wanayopokea kuto