Nike Air Zoom Alphafly Next% “Watermelon” kutua sokoni Julai 2 kwa Sh26,000
Na GEOFFREY ANENE
KAMPUNI ya vifaa vya michezo Nike yenye makao yake nchini Amerika itazindua viatu vipya vya Nike Air Zoom Alphafly Next% “Watermelon” mnamo Julai 2, 2020.
Viatu hivyo, ambavyo bei yake ni Sh26,626 (Dola 250 za Amerika), vinatumia teknolojia sawa sampuli ya viatu ambavyo bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge alivalia akiingia katika mabuku ya historia kwa kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili mwezi Oktoba 2019.
Mkenya huyo, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya saa 2:01:39 aliyoweka mjini Berlin nchini Ujerumani, alitimka mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 mjini Vienna, Austria mwezi Oktoba 2019.
Alitumia viatu vya aina ya Nike Zoom Vaporfly Next% mjini Vienna. Hakuna binadamu alikuwa amewahi kutimka mbio za kilomita 42 chini ya saa 2:00:00.
Viatu hivyo vimekumbwa na utata, hasa baada ya wakimbiaji waliovitumia kutimka muda mzuri mashindanoni.
Viatu vipya, ambavyo ni bora kuliko sampuli iliyotangulia, vitakuwa na rangi za tunda la tikiti maji (Watermelon).