NIKO SAWA! Arteta apona virusi hatari vya corona
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KOCHA Mkuu wa klabu ya Arsenal, Mikel Arteta amesema amepona virusi hatari vya corona, ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 8,000 na wengine 200,000 wakithibitishwa kuambukizwa kote duniani.
Wakati huo huo, Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Alhamisi iliahirishwa tena, wakati huu hadi Aprili 30 kutokana na janga hilo.
“Niko sawa, habari za punde ni kwamba hakuna virusi vya corona (mwilini). Namshukuru Mungu! Asanteni kwa sala zenu,” alisema kocha Arteta katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa Facebook, Alhamisi.
Arteta alipatikana na virusi vya corona, vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, juma lililopita na kusababisha mechi ya Jumamosi kati ya Arsenal na Brighton & Hove Albion kuahirishwa.
Aidha, wachezaji wote wa Arsenal pamoja na maafisa wa timu hiyo walilazimika kutengwa kwa siku 14 kwa sababu walikuwa wamefanya kazi kwa karibu na Arteta.
Karantini hiyo itatamatika Jumanne, na hali ikisalia kuwa shwari uwanja wao wa kufanyia mazoezi wa London Colney utafunguliwa tena na mazoezi kurejelewa.
Kupatikana kwa Arteta na virusi vya corona pia kulichangia uamuzi wa EPL kufutilia mbali ratiba nzima ya michuano hadi Aprili 3.
Hiyo jana, mechi hizo ziliahirishwa kwa majuma mengine zaidi na sasa hazitarejelewa hadi baada ya mwisho wa mwezi Aprili.
Katika kikao cha dharura cha bodi ya usimamizi wa soka nchini Uingereza (FA) hapo jana kupitia mtandao, maafisa hao pia waliafikiana kwamba michezo itakaporejea msimu wa 2019-2020 utasongezwa mbele hadi ligi ikamilike.
Kuahirishwa kwa Kombe la Bara Ulaya (Euro) 2020 kumepatia ligi za Bara Ulaya matumaini ya kumalizia misimu yao kabla ya mwisho wa mwezi Juni.
Hata hivyo, FA haikutarajiwa kutangaza tarehe mahususi ya kurejelea mazoezi kwa sababu uamuzi huo unategemea serikali ya Uingereza kuondoa marufuku dhidi ya mikusanyiko ya watu ili kuzuia uenezaji wa virusi hivyo.
Inaaminika kuwa marufuku hiyo isipoondolewa, maafisa watakubali mechi zisakatwe, lakini katika viwanja visivyo na mashabiki ili ratiba ya msimu huu ikamilike.
Kumekuwa na dalili kuwa klabu zimegawanyika kuhusu jinsi msimu unafaa kutamatika. Juma lililopita, naibu mwenyekiti wa West Ham, Karren Brady alisema msimu huu unafaa kufutiliwa mbali. Mwenyekiti wa FA, Greg Clarke pia alielezea wasiwasi wake kwamba huenda ikawa vigumu msimu kukamilika.
Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Brighton & Hove Albion, Paul Barber alinukuliwa na Shirika la Habari la BBC akisema kuwa ‘haitakuwa haki’ ikiwa viongozi Liverpool, ambao wamefungua mwanya mkubwa sana kati yao na nambari mbili (alama 25 zikisalia mechi tisa), watanyimwa taji. Barber pia alipendekeza idadi ya timu zinazoshiriki EPL iongezwe kutoka 19 hadi 22.
Wawakilishi wa klabu za ligi hiyo walitarajia kuonyeshwa njia mbalimbali ambazo msimu unaweza kutamatika na pia athari za kifedha na kisheria za njia hizo, wakati wa kikao cha jana.
Hata hivyo, kuna ari ya kuhakikisha msimu unakamilika ipasavyo. Ligi Kuu ilifanya mazungumzo na kampuni inayosimamia ligi zote nchini Uingereza (EFL) mnamo Jumatano. Pia inasemekana kuwa inazungumza na washirika wake wa kupeperusha mechi pamoja na wadhamini kuhusu uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Runinga za Sky na BT zimekataa kuzungumzia ripoti kuwa zitatafuta kulipwa fidia ya pauni 750 milioni ikiwa Ligi Kuu itavunja kandarasi ya pauni bilioni tatu ya kupeperusha mechi za nchini humo moja kwa moja. Klabu zinazoshikilia maeneo ya kuingia Ligi Kuu kutoka Ligi ya Daraja ya Pili zinasemekana pia ziko tayari kuelekea mahakamani ikiwa msimu utakatizwa na hivyo kuwanyimwa fursa ya kupandishwa ngazi