• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Nimechangia kuporomoka kwa taaluma ya Oezil – Arteta

Nimechangia kuporomoka kwa taaluma ya Oezil – Arteta

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amesema anahisi kwamba “alimwangusha” kiungo Mesut Oezil baada ya kumtema kwenye kikosi cha wanasoka 25 watakaotegemewa na klabu yake kwenye soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Europa League msimu huu.

Hatua hiyo ina maana kwamba Oezil ambaye ni mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani sasa ana uwezo wa kuchezea Arsenal U-23 pekee hadi mkataba wake utakapotamatika rasmi uwanjani Emirates mwishoni mwa msimu wa 2021.

Oezil, 32, alijiunga na Arsenal mnamo 2013 kwa kima cha Sh5.9 bilioni kutoka Real Madrid ya Uhispania. Nyota huyo aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia Ujerumani ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil, hajawahi kuwajibishwa na Arsenal kwenye mechi yoyote tangu Machi 7, 2020.

“Ambacho naweza kusema kwa upande wangu ni kwamba maamuzi ya kutomchezesha Oezil ni ya kisoka. Isieleweke kwamba sihusiani naye vizuri. Tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na anajua kinachotarajiwa kutoka kwake,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania.

“Kwa mchezaji wa hadhi ya Oezil ambaye anajivunia tajriba pevu kitaaluma, mambo mengi kumhusu husemwa hata kama tukio litakalomfanyikia ni dogo. Hali imekuwa hivyo kwake kwa miaka minane iliyopita. Vitu vingi vimefanyika na ninahisi kwamba nilichangia pia kuporomoka kwa makali yake,” akaongeza Arteta.

“Kazi yangu kwa sasa ni kuongoza kila mchezaji kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake uwanjani. Aimarike na ajikuze zaidi kitaaluma,” akaeleza.

Tangu ajiunge na Arsenal, Oezil amefungia Arsenal mabao 44 kutokana na mechi 254 katika mapambano yote.

Alianza kukosekana kwenye mipango ya Arsenal chini ya kocha Unai Emery kabla ya kurejea kikosini baada ya Freddie Ljungberg kuaminiwa fursa ya kushikilia mikoba ya Arsenal kabla ya kuja kwa Arteta.

Baada ya kuajiriwa kwa Arteta mnamo Disemba 2019, Oezil alipangwa kwenye mechi 10 za kwanza za EPL kabla ya janga la corona kusababisha kusitishwa kwa kipute hicho kuanzia Machi hadi Juni 2020.

Mnamo Oktoba, Oezil alijitolea kugharimia mshahara wa Jerry Quy ambaye amekuwa akitumika kama maskoti ya Gunnersaurus uwanjani Emirates kwa kipindi kirefu.

Hiyo ilikuwa baada ya Arsenal kufichua kwamba Guy, ambaye amekuwa akiwapa mashabiki na wachezaji burudani ya kipekee uwanjani kwa miaka 27 iliyopita, alikuwa sehemu ya vibarua 55 ambao watafutwa kazi baada ya hazina ya fedha ya Arsenal kulemwazwa na corona.

Ilivyo, Arteta aliamua kumtema Oezil kikosini mwake baada ya Arsenal kushindwa kumpa sogora huyo kitita kikubwa cha ujira anaostahili kupokezwa kwa mujibu wa mkataba wake ili atafute hifadhi mpya kwingineko.

Mechi ya mwisho kwa Oezil kuchezea Arsenal ni ile iliyoshuhudia kikosi hicho cha Arteta kikiwapokeza West Ham United kichapo cha 1-0 ligini mnamo Machi 7, 2020.

Japo Oezil atakuwa akishiriki mazoezi kambini mwa Arsenal, matumaini yake ya pekee ya kusakata soka msimu huu ni kuvalia jezi za kikosi cha U-23.

Oezil pia ana uhuru wa kuvunja ghafla uhusiano wake na Arsenal na kuingia katika sajili rasmi ya kikosi chochote kisichokuwa cha EPL kabla ya Oktoba 25, 2020, au kuwapa Arsenal barua ya kumruhusu ajiunge na klabu yoyote nyingine barani Ulaya katika muhula mfupi wa uhamisho wa wachezaji mnamo Januari 2021.

You can share this post!

Manaibu wa magavana sasa kupata sauti BBI ikipita

Uhuru azindua ujenzi wa uwanja mpya na wa kisasa mjini...