Nipe nikupe: Arsenal warusha chini Man City na kurejea tena juu ya mti wakisubiri jibu la Liverpool
NA FATUMA BARIKI
MIAMBA wa soka Arsenal wamerejea juu ya jedwali baada ya kupokeza Bighton mabao tatu kwa nunge katika mechi ya kusisimua ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Vijana hao wa kocha Mikel Arteta walianza mechi hiyo wakiwa nambari ya tatu, baada ya mahasimu wao katika kufukuzia taji la ligi Manchester City kupepeta Crystal Palace 4-2 awali, na kuonyesha The Gunners jinsi mlima ulivyokuwa ungali mrefu mbele yao.
Lakini Arsenal walienda ugani Amex wakiwa na motisha kubwa baada ya kukalifisha Luton Town katikati ya wiki kwa mabao mawili bila jibu.
Vijana wa Roberto De Zerbi walianza mechi hiyo kwa makeke, wakikalia ngumu kikosi cha Arsenal kisiweze kuachilia gozi lao rojorojo walivyozoea kwa muda sasa. Iliwajuzu kutumia muda mwingi kuzima ujanja wa Brighton ambao nao walikuwa na mori mkubwa sababu ya kucheza uga wa nyumbani.
Hata hivyo, mchezo ulifungukia Arsenal wakati mshambuliaji Gabriel Jesus alipoangushwa kwenye kisanduku, na ikawa ni penalti.
Bukayo Saka ambaye ameaminiwa katika kufunga mikwaju ya penalti alitenda kama alivyoajiriwa kufanya, na kuiweka timu yake kifua mbele.
Kipindi cha kwanza kikaisha hali ikiwa moja nunge, na mchezo uliporejelewa kwa kipindi cha pili, wasiwasi ulianza kuwaingia The Gunners kwa jinsi bado walisomwa sana mchezo wao na kukosa mianya ya kupenya.
Kufikia dakika ya 65, ilikuwa dhahiri kwamba iwapo hawangepata bao la pili la kuwahimili, basi walikuwa wakabiliwe na wakati mgumu zaidi kwa sababu Brighton wanafahamika kukoleza mashambulizi katika dakika za lala salama.
Lakini Arsenal wakapiga moyo konde na wakajaribisha tena mchezo wao wa pasi rojorojo na mojawapo ya pasi hizo zikazaa bao la pili lililofungwa na Kai Havertz aliyeandaliwa krosi moto na Jorginho.
Bao la tatu nalo likawa kama vile lilikuwa limeandikwa kwenye vitabu, kwamba Leandro Trossard atafunga dhidi ya kikosi kilichomlea kitaaluma kabla ya kununuliwa na Arsenal.
Sasa ‘Ndovu’ Arsenal wanaselelea kwenye juu ya jedwali kwa alama 71, moja zaidi ya Liverpool ambao wanaonana na miamba wengine Manchester United ugani Old Trafford, Jumapili.