• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Nipeni mamilioni yangu tuachane roho safi – Migne

Nipeni mamilioni yangu tuachane roho safi – Migne

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa Harambee Stars, Sebastien Migne yuko tayari kutengana na Kenya muradi tu Shirikisho la Soka nchini (FKF) limlipe kila kitu katika kandarasi yake ya miaka mitatu itakayotamatika Juni 30, 2021.

Mfaransa huyu ambaye hupokea mshahara wa Sh1.5 milioni kila mwezi, amejipata akikabiliwa na presha kutoka kwa mashabiki wa Kenya.

Wanataka afurushwe baada ya Stars kubanduliwa nje ya Kombe la bara Afrika la soka ya wachezaji wanaocheza katika mataifa yao almaarufu CHAN, Jumapili.

Alisema baada ya mechi, “Kama FKF inataka kunitimua, niko tayari, lakini kama kulipa mshahara wangu ni tatizo, sasa itaweza kulipia kandarasi yangu kweli?” aliuliza.

Vijana wa Migne walizidiwa maarifa na Tanzania katika upigaji wa penalti 4-1 baada ya dakika 180 kumatika bila bao. Wakenya walisalia na masikitiko pamoja na maswali magumu baada ya timu yao kushindwa kuendeleza ubabe wake dhidi ya Tanzania siku 39 tu baada ya kuchapa majirani hao 3-2 katika mechi ya makundi ya Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri.

Maswali kama ‘Nani aliyeroga Harambee Stars?’, ‘Sababu ya Harambee Stars kufanya vibaya ni nini?’ na ‘Mnapokuwa na kocha asiyefahamu kitu, mnatarajia kupata nini?’ yameulizwa na mashabiki waliojaa hasira kutokana na matokeo ya hivi punde.

Kenya, ambayo haijawahi kushiriki mashindano ya CHAN tangu yaanzishwe mwaka 2009, ilikaba Tanzania 0-0 jijini Dar es Salaam mnamo Julai 28.

Wakenya walijawa na imani vijana wa Migne watumia ardhi ya nyumbani, uwanjani Kasarani, kukamilisha kazi. Hata hivyo, mambo yalikuwa magumu.

Penalti

Baada ya dakika zingine 90 kukamilika bila bao, mikwaju ya penalti ililazimika kutumika kuamua timu itakayoingia katika raundi ya pili kulimana na Sudan ili kufuzu kushiriki CHAN mwaka 2020.

Hapa ndipo Kenya ilifeli mtihani vibaya.

Clifton Miheso pekee ndiye alifuma wavuni penalti yake, huku Michael Kibwage, Samuel Onyango, Joash Onyango wakipoteza zao.

Tanzania, ambayo ilishiriki makala ya kwanza ya CHAN nchini Ivory Coast, iliweka hai matumaini ya kurejea katika mashindano haya ilipomwaga kipa John Oyemba kupitia penalti za Jonas Mkudde, Paulo Nyanganya, Gabriel Kamagi na Aiyee Hamis.Baada ya kutupwa nje kupitia mikwaju ya penalti, Wakenya walijitosa kwenye mitandao ya kijamii kulaumu Migne.

Naibu kocha Francis Kimanzi na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa, pia hawakuepuka hasira ya mashabiki.

Shabiki Reinhard Maloney alisema, “Mnapokuwa na kocha asiyefahamu kitu, mnatarajia nini? Kucheza na mshambuliaji mmoja mkiwa nyumbani kulionyesha kabisa aina ya kocha tumeajiri.”

Bev Bev, “Sebastian Migne ana kiburi sana…anafaa kukaa kando ama kupigwa kalamu! Sioni tofauti ya makosa tuliyoyafanya katika Kombe la Afrika (AFCON) na haya nimeona leo.”

Kilonzo Manuvah akasema, “Sebastian Migne si kocha mstahiki wa Harambee Stars.”

Naye Patrick Kim anashauri, “Shughulikieni kocha huyu anayependa kutumia mbinu za kuzuia na Harambee Stars itaenda mbali.”

Davidenko Katamesh ni mmoja wa mashabiki wachache waliokuwa na maoni tofauti sana. Alitetea benchi la kiufundi akisema, “Wakati huu ni wa kukosoa wachezaji. Si kila kichapo kinasababishwa na kocha.”

Vitisho vya Migne huenda vikaifanya FKF kupiga hatua moja nyuma kabla ya kuwazia kumpiga kalamu. Inafahamu bado makocha wa zamani Adel Amrouche na Bobby Williamson wanadai Kenya Sh132 milioni na Sh145 milioni mtawalia. Kandarasi zao zilitamatishwa kabla ya muda wao kumalizika. Mashabiki wa Kenya wanapendekeza Amrouche apewe majukumu ya Migne.

  • Tags

You can share this post!

Lazima tujipange kabla ya mechi za marudiano – Odera

SHANGAZI AKUJIBU: Aliyenioa hanipendi, sijui nihamie kwa...

adminleo