Michezo

Nitajiamulia mwenyewe siku ya kuondoka Arsenal – Ozil

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Mesut Ozil wa Arsenal amesema atasalia kuhudumu uwanjani Emirates hadi siku ya mwisho ambapo mkataba wake na kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta utatamatika rasmi mnamo Juni 2021.

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, hajawajibishwa na Arsenal tangu kurejelewa kwa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 17, 2020, huku Arteta akishikilia kwamba kiini cha hatua hiyo ni “sababu za kimkakati zilizochochewa na mahitaji ya kila mchuano”.

Ozil, 31, pia amepuzilia mbali tetesi kwamba Arsenal wanapanga kumlipa kwa mwaka mzima kiasi chote cha malipo ya Sh49 milioni kwa wiki ili aondoke.

“Mambo yamekuwa magumu kwangu lakini sina nia ya kuagana na Arsenal kwa sababu ni kikosi kinachokipenda sana. Nitaamua pa Kwenda siku ikifika, sitakubali hatima yangu kitaaluma kuamuliwa na watu wengine,” akasema kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid.

“Nitajitolea kadri ya uwezo wangu kuwajibikia Arsenal katika vibarua vyote vilivyopo mbele yao. Hali ya sasa inayonikabili uwanjani Emirates haitavunja azma yangu. Itachangia tu katika kunikomaza. Niliwahi kudhihirisha hapo awali kwamba nina uwezo wa kurejea katika kikosi cha kwanza na nipo tayari kufanya hivyo,” akaongeza.

Ozil alijiunga rasmi na Arsenal mnamo 2013 baada ya kuagana na Real kwa kima cha Sh5.9 bilioni. Hata hivyo, alifarakana na kocha Unai Emery kabla ya kuanza kupangwa tena kwenye kikosi cha kwanza chini ya mkufunzi Freddie Ljungberg aliyeshikilia mikoba ya The Gunners kabla ya kuajiriwa kwa Arteta.

Baada ya Arteta kupokezwa mikoba ya Arsenal mnamo Disemba 2019 Ozil alipangwa katika kikosi cha kwanza kwenye mechi zote 10 za kwanza za EPL kabla ya janga la corona kulazimisha kipute hicho kuahirishwa kwa miezi mitatu zaidi mnamo Machi 20120.

Hata hivyo, hajawajibishwa kabisa katika mechi 13 zilizopita katika mashindano yote ya hadi kufikia sasa.

Licha ya Arteta na wanasoka wengine wa Arsenal kukubali kunyofolewa mshahara kwa asilimia 12.5, Arsenal walifuta kazi wafanyakazi 55 wiki hii kwa madai kwamba janga la corona lilitikisa pakubwa hazina yao ya fedha.

Ozil aliyekataa kupungiziwa mshahara mnamo Aprili 2020 na anahisi kwamba maamuzi ya kutochezeshwa kwake huenda yalichangia na hatua yake hiyo.

Japo amesema kwamba anaheshimu maamuzi ya Arteta ya kumwacha nje ya kikosi cha kwanza cha Arsenal katika mechi zote za tangu Juni 17, Ozil amesema kwamba anastahili kupewa nafasi ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake.

“Huwezi kukosa jumla ya mechi 13 mfululizo iwapo wewe si mgonjwa, hujivunii fomu nzuri, huna matatizo ya utovu ya nidhamu au kisu cha makali yako yamesenea tu kabisa ukawa kisu butu kilichoingia kutu,” akasema Ozil kwa kusisitiza kuwa licha ya kwamba yeye hakuwa mchezaji wa pekee aliyekataa kupunguziwa posho, ni jina lake pekee ndilo lililotolewa katika taarifa ya Arsenal kwa vyombo vya habari.