Michezo

Nketiah ainusuru Arsenal kutoka kwa nyundo la West Ham

September 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta alikuwa mwingi wa sifa kwa ukakamavu wa kikosi chake baada ya chipukizi Eddie Nketiah kufunga bao la dakika za mwisho lililowavunia Arsenal ushindi wa 2-1 dhidi ya West Ham United mnamo Septemba 19, 2020.

Mchuano huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa West Ham United kupoteza na ni mara yao ya tatu katika kipindi cha misimu minne iliyopita kupoteza mechi mbili za kwanza za msimu mpya.

“Nilipendezwa na ari ya vijana wangu katika dakika 25 za mwisho. Walijitahidi sana kujinyanyua baada ya wapinzani kuwasakama na kuonekana kuwazidi nguvu katika takriban kila idara,” akatanguliza Arteta.

“Pengine miezi michache iliyopita, huo ni mchuano ambao tungeambulia sare au hata kupoteza. Lakini tulishinda. Mwishowe, itatulazimu kubuni mbinu za kukabili mechi za aina hiyo kwa sababu zitakuwepo kwa wingi msimu huu,” akaongeza kocha huyo raia wa Uhispania.

Arsenal walitamba katika dakika za mwanzo za mchuano huo na wakajipata kifua mbele kupitia bao la Alexandre Lacazette aliyekamilisha krosi ya Pierre-Emerick Aubameyang kwa kichwa.

Ingawa hivyo, West Ham walikuwa tishio kila walipopata mipira ya kushtukiza na wakasawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia Michail Antonio aliyeshirikiana vilivyo na Ryan Fredericks.

Ingawa Arsenal waliendelea kumiliki asilimia kubwa ya mpira mwanzoni mwa kipindi cha pili, masogora wa kocha David Moyes ndio walijivunia nafasi nyingi za kufunga mabao na Antonio akashuhudia mpira aliougonga kwa kichwa ukibusu mwamba wa goli la wenyeji wao.

Fowadi huyo alinyimwa pia nafasi ya wazi na kipa Bernd Leno ambaye sasa ana uhakika wa kuwa chaguo la kwanza la Arsenal baada ya Emiliano Martinez kuyoyomea Aston Villa.

Ushirikiano kati ya Nketiah na Dani Ceballos mwishoni mwa kipindi cha pili uliwapa Arsenal bao la ushindi. Bao hilo liliendeleza rekodi nzuri ya Arsenal ambao kwa sasa wamesajili ushindi mara 11 kutokana na mechi 12 zilizopita dhidi ya West Ham ugani Emirates.

Japo Arsenal wameonekana kufufua makali yao chini ya Arteta tangu Disemba 2019, uthabiti wao uliyumbishwa na West Ham baada ya Lacazette kuondolewa katika dakika ya 77 na nafasi yake kutwaliwa na Nketiah.

Sajili mpya Willian Borges alitolewa ugani katika dakika ya 66 na nafasi yake kuchukuliwa na Nicolas Pepe ambaye pia alishindwa kuamsha kasi ya mashambulizi ya Arsenal.

Bao la Lacazette katika gozi hilo lilikuwa lake la 50 akiwa ndani ya jezi za Arsenal waliomsajili miaka mitatu iliyopita kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO