Michezo

Nondies wajinasia huduma za wanaraga watano matata

December 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Nondies kimesajili wanaraga watano kadri kinavyozidi kujisuka upya kwa kampeni za msimu mpya wa 2020-21 katika Ligi Kuu ya Kenya Cup.

Mbali na Daniel Taabu aliyeagana na Mwamba RFC, wanaraga wengine wapya ambao wameingia katika sajili rasmi ya Nondies ni Samuel Motari na Kelvin Kanyiri waliobanduka kambini mwa Impala Saracens. Weingine ni Charles Omondi aliyeondoka Homebyz RFC na Brian Simiyu aliyekatiza uhusiano wake na kikosi cha Northern Suburbs.

Kocha Willis Ojal amefurahishwa na kiwango cha ubora wa wachezaji hao na ameeleza ukubwa wa matumaini ya kutua ndani ya mduara wa tano-bora na hatimaye kunyanyua ubingwa wa taji la msimu wa 2021-22.

“Wanaleta nguvu mpya, tajriba pevu na uzoefu mpana ambao naamini utazidisha ushindani mkali utakaotukweza pazuri mwishoni mwa kampeni za msimu ujao,” akasema.

Nondies kwa sasa hushiriki vipindi vitatu vya mazoezi kwa wiki – Jumanne, Alhamisi na Jumamosi katika makundi ya wachezaji 20 uwanjani Ngong Racecourse.

Katika kampeni za msimu uliopita, Nondies waliambulia nafasi ya saba na kukosa fursa ya kufuzu kwa hatua ya mwondoano.

“Kikosi kwa sasa kinajivunia mseto mzuri wa wachezaji wazoefu na chipukizi wenye kasi ya ajabu. Tunalenga sasa kuoanisha mitindo ya kucheza kwao na kufanya Nondies kuwa miongoni mwa vikosi thabiti zaidi ligini,” akaongeza Ojal.

Nondies wanasajili wanaraga watano miezi michache baada ya kuongeza Hillary Itela, Michael Aung na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 almaarufu ‘Chipu’ kwenye benchi yao ya kiufundi.

Nondies wanajivunia kutwaa idadi kubwa zaidi ya mataji ya Kenya Cup (17) na Enterprise Cup (24). Hata hivyo, walitawazwa wafalme wa Kenya Cup kwa mara ya mwisho mnamo 1998.

Miongoni mwa wanaraga tegemeo kambini mwa Nondies kwa sasa ni Ian Mabwa, Brian Sinei, Ina Njenga na nahodha Steve Odhiambo.