Michezo

NRG Radio pabaya kwa 'kudandia' jina la Kipchoge

October 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KITUO cha NRG Radio, ambayo inapatikana katika jumba la Almont Park kwenye barabara ya Church Road mtaani Westlands jijini Nairobi, imejipata pabaya baada ya kutumia jina la mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon, Eliud Kipchoge kujiuza.

Kipchoge, ambaye ni mtu wa kwanza duniani kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili baada ya kutimka mbio za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 nchini Austria mnamo Oktoba 12, alitisha kushtaki kituo hicho kilipotumia jina lake kujipiga debe bila idhini yake.

Kupitia wakili wake Donald Kipkorir, mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 34, alisema Ijumaa kuwa amepatia NRG Radio saa mbili kuondoa jina lake, picha na kitu chochote kinachomgusia katika mitandao yake yote ya kijamii. Pia, redio hiyo imeamrishwa kuomba msamaha kwa kuvunja haki zake na kutumia vibaya jina lake, picha na sifa yake.

“Tumefahamishwa na mteja wetu Eliud Kipchoge kuwa bila ruhusa yake, mamlaka na leseni mmebadilisha sehemu ya juu ya kurasa zenu za mitandao ya kijamii na blogu zenu kuwa Kipchoge Radio na KipchogeRadioNRGRadioKenya. Bila ya ruhusa ya mteja wetu, mlidanganya wasikilizaji na wafuasi wenu kuwa kwa kuwafuata kwenye Instagram, mtapatia mteja wetu gari. Mteja wetu hakuitisha wala hahitaji zawadi yoyote ya gari kutoka kwenu ama gari lolote,” ilisema barua kutoka kwa wakili huyo kwa shirika hilo la utangazaji.

Inasemekana kuwa NRG Radio ilibadilisha jina lake na kuwa ‘Kipchoge Radio’ na kuendesha shindano kwenye mitandao yake ya kijamii kwa karibu wiki moja ikiahidi kutunuku Kipchoge gari la aina ya BMW i8 iwapo wafuasi wa redio hiyo kwenye Instagram wangefika milioni moja kufikia Oktoba 17.

Redio hiyo imeondoa jina la Kipchoge na sasa inajiita Mashujaa Radio.

Haijulikani kama imeomba msamaha kwa sababu hakuna ripoti imefanya hivyo.