Nusra Man City imuue Ndovu ikimshusha juu ya mti
NA MWANGI MUIRURI
ARSENAL iliponea chupuchupu katika kipute chake na Man City Jumapili jioni, Machi 31, 2024 huku timu zote mbili zikisaka ubabe wa ligi kuu ya Uingereza.
Arsenal ambayo katika siku za hivi majuzi imejipa jina la majazi la Ndovu ilihemeshwa na kuwekwa chini ya shinikizo, nusura iage dunia kwa kutoleshwa kijasho bila huruma.
Lakini bahati ya mtende ndiyo ilikuwa rafiki wa dhati kwa ndovu, huku umiliki wake wa mpira ukiwa ni asilimia 27 pekee dhidi ya Man City iliyoiweka guuni kwa asilimia 73.
Man City iliachilia mashuti 12 kusaka mabao, nayo Arsenal ikifanikiwa mara sita.
Mashuti yaliyolenga michuma ya Man City yalikuwa ni moja pekee, Arsenal ikilenga kihafifuhafifu mara mbili.
Arsenal ambayo husifika kwa kutandaza pasi tamu katika kila pembe ya uwanja kwa mtanange huu ilibaki hoi na ilifanikiwa tu kuonana mara 269, wapinzani wakionana mara 700.
Hii ina maana kwamba kwa kila dakika Arsenal ilikuwa ikionana mara 3, Man City ikionana mara 8.
Katika kuonana huko kwa pasi, uhakika wa Arsenal ulikuwa asilimia 71 huku wa Man City ukiwa asilimia 88.
Licha ya kuonekana kuchezewa ngware mara kwa mara, Arsenal ndiyo ilikuwa bingwa wa visivyo kwa 20 dhidi ya 9 za Man City.
Ngware hizo za Arsenal ziliishia kadi mbili za manjano huku Man City ikikosa hata moja, timu zote mbili zikikosa kadi nyekundu hata moja.
Man City iliotea mara mbili, Arsenal ikifanya hivyo mara moja.
Aidha, Man City wakinolewa na kocha Pep Guardiola ilipata kona 7, Arsenal ya Mikel Arteta ikipata zake 4.
Matokeo hayo yakaiacha ndovu ikishuka kutoka juu ya mti hadi chini ya meza kwa pointi 65 nayo Man City ikidumisha nafasi yake ya tatu kwa pointi 64.
Liverpool ambayo hapo awali ilikuwa imeadhibu Brighton kwa mabao 2-1 ilipanda juu ya mti kwa pointi 67.
Mkambano huo mkali unazidi kushuhudiwa, huku timu hizo tatu zikisalia na mechi 9 kila moja, hizo zikiwa ni pointi 27 za kushindania.