Nuttal apigwa kalamu Ghana kuhusu ufisadi
Na CECIL ODONGO
ALIYEKUWA kocha mkuu wa klabu ya Gor Mahia, Frank Nuttal hatimaye amefutwa kazi na klabu ya soka nchini Ghana, Hearts of Oak kutokana na madai ya kushiriki ufisadi.
Nuttal alisimamishwa kazi siku saba zilizopita huku kamati ya uchunguzi ikizamia madai dhidi yake na kumpata na hatia. Sasa wameamua kumfurusha kabisa kama kocha.
Kocha huyo anakabiliwa na madai mazito ya kupokea zaidi ya Sh5 milioni kwenye mchakato haramu ya kuuzwa kwa wachezaji wa timu hiyo.
Kulingana na taarifa kutoka kwa klabu hiyo, kocha huyo anasemekana kuomba radhi kwa kitendo hicho mbele ya kamati ya uchunguzi na kusikitia kosa lake la kutofahamisha uongozi wa klabu hiyo kuhusu swala hilo. Hata hivyo, hilo halikufanya asiangukiwe na shoka la kutemwa.
Bw Nutall alikuwa kocha wa Gor Mahia kati ya mwaka wa 2015-2016 kabla ya kuagana na mabingwa hao wa KPL na kuyoyomea klabu ya Zamalek FC kule Misri kama naibu kocha.
Katika kipindi hicho alisaidia mabingwa hao kuyatia kapuni mataji mawili ya ligi, kombe la Dstv Super CUP, KPL Top Eight na kuwafikisha kwenye fainali ya CECAFA Kagame cup walikopoteza dhidi ya klabu ya Azam ya Tanzania. Pia alitajwa kama kocha bora wa msimu wa 2015 humu nchini.