Nyani Iker Casillas asema 'tosha gari' katika ulingo wa soka
Na CHRIS ADUNGO
NAHODHA na kipa Iker Casillas aliyewaongoza Uhispania kutwaa Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini, amestaafu rasmi kwenye ulingo wa soka.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 ameangika glavu zake wiki moja baada ya mkataba wake na FC Porto ya Ureno kutamatika mnamo Juni 30, 2020.
Casillas aliwahi kupata maradhi ya moyo akiwa katika kambi ya mazoezi ya Porto mnamo Aprili 2019. Tangu wakati huo, hajawajibishwa kabisa katika mchuano wowote licha ya kujumuishwa mara kwa mara katika kikosi cha akiba.
Baada ya kupona, alipokezwa baadhi ya majukumu mepesi katika benchi ya kiufundi ya Porto mnamo Julai 2019 huku akisaidiana pia na wakufunzi wanawanoa makipa wa kikosi chipukizi.
Mnamo Februari 2020, Rais wa Porto, Jorge Nuno Pinto da Costa alisema kwamba Casillas alitazamiwa kustaafu mapema kambini mwao ili kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF).
Hata hivyo, alijiondoa katika kivumbi hicho cha kuwania urais wa RFEF, akisisitiza kuwa maamuzi hayo yalichangiwa na hali mbaya ya sasa inayotishia maendeleo ya Uhispania kijamii, kiuchumi na kiafya tangu kulipuka kwa virusi vya homa kali ya corona.
Hadi kufikia Julai 4, 2020, zaidi ya watu 28,000 walikuwa wameaga dunia nchini Uhispania kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
“Ripoti hizi ni za kuvunja moyo. Sioni tija na fahari yoyote kuwania kiti cha urais wa RFEF wakati ambapo taifa linapitia changamoto nyingi za kila sampuli katika sekta zote” akasema Casillas.
Kujiondoa kwa Casillas kunamsaza Rais wa sasa wa RFEF, Luis Rubiales katika nafasi maridhawa ya kuchaguliwa tena bila kupingwa kwa muhula mpya wa miaka minne katika uchaguzi utakaoandaliwa mnamo Agosti 2020.
Mbali na kuongoza Uhispania kunyakua taji la kwanza la Kombe la Dunia mnamo 2010, Casillas alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Uhispania kilichotwaa ubingwa wa Euro 2008 na 2010.
Aliingia katika sajili rasmi ya Porto mnamo 2015 baada ya kuhudumu kambini mwa Real Madrid, Uhispania kwa miaka 25.
Akiwa Porto, Casillas aliwajibishwa katika jumla ya mechi 156 na akawasaidia kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Ureno mnamo 2017-18.