Nyota wa klabu za 'majuu' kutegemewa Kenya dhidi ya Zambia kirafiki
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO Francis Kahata wa Simba SC nchini Tanzania na kipa Ian Otieno wa Zesco United nchini Zambia, ndio wanasoka wa kwanza wanaochezea ughaibuni kuingia kambini mwa Harambee Stars kwa minajili ya mechi ijayo ya kirafiki dhidi ya Chipolopolo ya Zambia.
Stars kwa sasa wanashiriki mazoezi uwanjani MISC Kasarani na watashuka dimbani kuvaana na Zambia mnamo Oktoba 9, 2020, ugani Nyayo, Nairobi kabla ya kupepetana na Comoros katika mechi mbili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 mwezi ujao wa Novemba 2020.
Ujio wa Kahata, Otieno na kiungo Anthony ‘Teddy’ Akumu wa Kaizer Chiefs nchini Afrika Kusini, unatarajiwa kupiga jeki maandalizi ya Stars ambao wamepangwa na Comoros, Misri na Togo kwenye Kundi G la kufuzu kwa AFCON nchini Cameroon mnamo 2021.
Wanasoka wengine wanaotandaza soka ya kulipwa katika mataifa ya nje ambayo wamewasili humu nchini ni Clarke Oduor (Barnsley, Uingereza) na Cliff Nyakeya (Masr FC, Misri).
Kahata alikuwa sehemu muhimu katika kampeni za Simba SC waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania mnamo 2019-20.
Nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia alikuwa pia tegemeo kubwa la Stars kwenye fainali za AFCON zilizoandaliwa nchini Misri mnamo 2019.
Kenya walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.
Jumla ya wanasoka 11 wanaochezea klabu mbalimbali za humu nchini walikuwa wameripoti kambini mwa Stars na kufanyiwa vipimo vya corona hadi wachezaji hao watano wanaosakata kabumbu katika mataifa ya kigeni kufika humu nchini.
Wanasoka zaidi walitarajiwa kambini mwa Stars kufikia mwisho wa Oktoba 6, 2020, japo kocha Francis Kimanzi atakosa huduma za kipa Arnold Origi, kiungo Eric Johanna, fowadi Michael Olunga na nahodha Victor Wanyama.
KIKOSI CHA KENYA:
MAKIPA: Ian Otieno (Zesco United), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars);
MABEKI: Brian Mandela (hana klabu), Johnstone Omurwa (Wazito), Joash Onyango (Simba), Joseph Okumu (Elfsborg, Uswidi), Clarke Oduor (Barnsley, Uingereza), David Owino (Mathare United), Philemon Otieno (Gor Mahia), Badi Baraka (KCB);
VIUNGO: Kenneth Muguna (Gor), Francis Kahata (Simba, Tanzania), Cliff Nyakeya (Masr FC, Misri), Anthony Akumu (Kaizer Chiefs), Hassan Abdalla (Bandari), Lawrence Juma (Gor), Katana Mohammed (Isloch, Belarus), Austin Otieno (AFC Leopards);
WAVAMIZI: Elvis Rupia (AFC Leopards), Masoud Juma (JS Kabylie, Algeria), Timothy Otieno (Napsa Stars, Zambia), Oscar Wamalwa (Ulinzi Stars).