Michezo

NYOTA WA WIKI: Jadon Sancho

May 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA GEOFFREY ANENE

JADON Sancho alitawazwa mchezaji bora na tovuti ya Flashscore wakati Borussia Dortmund ilinyuka Paris Saint-Germain 1-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (Uefa), mnamo Jumatano usiku.

Pia, Mwingereza huyo mwenye asili ya Trinidad & Tobago alitiwa katika timu ya wiki ya Uefa na tovuti ya takwimu za soka ya WhoScored.com kufuatia mchezo wake wa kufana ugani Signal Iduna Park wiki hii.

Ingawa hakujumuishwa kwenye timu ya wiki ya Uefa ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Sancho aliridhisha wengi wakiwemo majagina Erik ten Hag, Ally McCoist na Thierry Henry.

Katika mechi hiyo, Sancho alidhihirisha ni mzuri katika kulisha wapinzani chenga, kudhibiti mpira, kusuka pasi, kuchota pasi za kufungua safu ya ulinzi na pia kutoa pasi muhimu.

Sancho aliyekuwa shabiki mkubwa wa Chelsea na wachezaji Ronaldinho na Frank Lampard akiwa mtoto, alianza soka mapema.

Hata hivyo, alipata mwelekeo mzuri kwa kujiunga akademia ya Watford akiwa na umri wa miaka saba.

Alinyakuliwa na Manchester City mwaka 2015 kabla ya kugura miamba hao akitafuta nafasi katika kikosi cha kwanza na kujiunga na Dortmund mwaka 2017.

Hakusikitisha nchini Ujerumani akivutia Manchester United iliyomwaga Sh12.3 bilioni (pauni 73 milioni) mwezi Julai 2021 na kumpa kandarasi ya miaka mitano.

Sancho anayelinganishwa kimchezo na Ferran Torres (Barcelona) na Kaoru Mitoma (Brighton), alikosana na Ten Hag mapema Septemba 2023 na kupoteza nafasi yake mwezi huo kwa kukataa kuomba msamaha.

Alijiunga na Dortmund mwezi Januari 2024 ambako amefufua mchezo wake.

Kimataifa, Sancho, ambaye shujaa wake ni supastaa Mreno Cristiano Ronaldo, ameshirikishwa katika kikosi cha watu wazima cha Uingereza mara 23 tangu Oktoba 2018 na kuifungia mabao matatu.

Akiendelea kuridhisha huenda akapata namba katika kikosi cha kocha Gareth Southgate cha Kombe la Ulaya litakalofanyika Juni 2024.

Ana asili ya Trinidad & Tobago alikotoka mama yake naye baba yake ana mizizi nchini Jamaica na Guyana.

Itakumbukwa Sancho alikuwa katika kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 waliotawala Kombe la Dunia 2017.

Ajenti wa Sancho, Emeka Obasi pia anasimamia beki Mkenya Joseph Okumu anachezea Stade Reims nchini Ufaransa.