Michezo

Nyumba ya Fabinho yavunjwa, gari lake laibwa

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

NYUMBA ya kiungo wa Liverpool, Fabinho Henrique Tavares, 26, ilivamiwa wakati alipokuwa uwanjani na wenzake kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 30 mnamo Julai 22, 2020.

Wezi walivamia makazi ya kiungo huyo mzawa wa Brazil katika eneo la Formby viungani mwa jiji la Merseyside, Uingereza na kuiba mapambo ya thamani kubwa na gari aina ya Audi RS6. Gari hilo lilipatikana baadaye limeegeshwa kando ya barabara mjini Wigan, Uingereza.

Wizi katika makazi hayo ya Fabinho uligunduliwa aliporejea nyumbani baadaye kutoka uwanjani alikokuwa na familia yake kwa minajili ya gozi dhidi ya Chelsea kabla ya sherehe za kutawazwa kwao wafalme wa EPL kwa mara ya kwanza tangu 1990.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi jijini Merseyside, wezi walikuwa awali wamelenga kulivamia boma la Fabinho kati ya saa kumi na moja jioni ya Jumatano ya Julai 22, 2020 na saa kumi na mbili alfajiri ya Alhamisi ya Julai 23, 2020.

Mnamo Julai 22, 2020, Sir Kenny Dalglish, aliwapokeza Liverpool kombe la EPL msimu huu baada ya ushindi wao wa 5-3 dhidi ya Chelsea uwanjani Anfield.

Fabinho aliingia katika sajili rasmi ya Liverpool mnamo 2018 baada ya kuagana rasmi na AS Monaco ya Ufaransa. Amewahi pia kuvalia jezi Real Madrid ya Uhispania kati ya 2012 na 2013.