• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Obiri aambulia pakavu mbio za mita 3,000 Birmingham

Obiri aambulia pakavu mbio za mita 3,000 Birmingham

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilianza kampeni yake kwenye Riadha za Dunia za Ukumbini kwa masikitiko baada ya nyota Hellen Obiri kutoka mikono mitupu katika mbio za mita 3,000 mjini Birmingham nchini Uingereza, Alhamisi usiku.

Malkia wa mbio za mita 5,000 za nje ya ukumbi duniani Obiri alikuwa amepigiwa upatu kushinda medali.

Hata hivyo, bingwa huyu wa mwaka 2012, ambaye aliridhika na medali ya fedha mwaka 2014 mjini Sopot nchini Poland, alikamilisha katika nafasi ya nne mjini Birmingham.

Muethiopia Genzebe Dibaba aliongeza ubingwa wa mwaka 2018 kwa mataji aliyonyakua mwaka 2014 na 2016 aliposhinda taji lake la tatu kwa dakika 8:45.05. Mjerumani Konstanze Klosterhalfen aliongoza mita 2000 za kwanza kabla ya Dibaba kuchukua usukani na kusalia kileleni hadi mwisho.

Obiri, ambaye hakushiriki makala ya mwaka 2016, alimaliza katika nafasi ya nne kwa dakika 8:49.66, huku medali za fedha na shaba zikinyakuliwa na mzawa wa Ethiopia Sifan Hassan (Uholanzi) na Laura Muir (Uingereza), mtawalia.

Kenya inawakilishwa na wakimbiaji saba katika mbio nane mjini Birmingham. Bethwell Birgen, David Kiplangat (mita 3000), Emmanuel Korir (mita 800), Beatrice Chepkoech (mita 1500) na Winny Chebet (mita 800 na mita 1500) wamepangiwa kuanza kampeni yao Ijumaa. Vincent Kibet atafungua kampeni yake Jumamosi katika mbio za mita 1500.

Matokeo ya mbio za mita 3,000 (Machi 1, 2018):

Genzebe Dibaba (Ethiopia) dakika 8:45.05

Sifan Hassan (Uholanzi) 8:45.68

Laura Muir (Uingereza) 8:45.78

Hellen Obiri (Kenya) 8:49.66

Shelby Houlihan (Marekani) 8:50.38

Fantu Worku (Ethiopia) 8:50.54

Konstanze Klosterhalfen (Ujerumani) 8:51.79

Katie Mackey (Marekani) 8:56.62

Dominique Scott (Afrika Kusini) 8:59.93

Eilish McColgan (Uingereza) 9:01.32

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 10, 2018

‘Babu Owino’ na mlinzi wake waonywa na mahakama

adminleo