Oduor, 20 kusakata soka Uingereza kwa miaka 4
Na JOHN KIMWERE
MKENYA Clarke Sydney Omondi Oduor aliibuka miongoni mwa wanasoka wawili walionaswa na Barnsley FC ya Uingereza siku moja kabla ya kukamilika kwa kipindi cha uhamisho.
Chipukizi huyo walisajiliwa wakati mmoja na Patrick Schmidt raia wa Australia. Usajili huo unatoa nafasi kwa chipukizi huyo kuorodheshwa miongoni mwa wasajili wapya 12 watakaosakatia klabu hiyo muhula huu.
Oduor mwenye umri wa miaka 20 tayari ametia wino kandarasi ya miaka minne kusakatia klabu hiyo kwenye kampeni za soka la daraja ya pili akitokea Leeds United ambayo pia hushiriki kipute hicho.
Kulingana na habari ambazo zimechapishwa katika mtandao wa Barnsley, mchezaji huyo alichukua hatua hiyo baada ya viongozi wa klabu hiyo kutangaza kwamba wanahitaji huduma zake. ”Nina furaha tele kujiunga na klabu itakayonipa nafasi kuonyesha uwezo wangu uwanjani,” Oduor akasema.
Alipokuwa mali ya Leeds United alibahatika kuichezea mara moja alipoingia dimbani kipindi cha pili kama nguvu kwenye mechi ambayo klabu hiyo iliteleza na kukungútwa mabao 2-1 na Queens Park Rangers (QPR) msimu uliyopita.
Talanta ya mchana nyavu huyo aligunduliwa akipigia kikosi cha Leeds United Academy baadaye mwaka 2017 alitwalia na Leeds United ya wakomavu.