• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
Okari achezea Bakken Bears ikipigwa vikapuni Denmark

Okari achezea Bakken Bears ikipigwa vikapuni Denmark

NA MASHIRIKA

BAKKEN Bears Aarhus, ambayo imeajiri Mkenya Tylor Okari Ongwae, imekamilisha mechi za kupima nguvu kwa kichapo Alhamisi kabla ya kuanza kampeni ya kuingia Klabu Bingwa ya Mpira wa Vikapu barani Ulaya hapo Septemba 23.

Bears ilianzisha Ongwae pamoja na Justin Dentmon, Darko Jukic, Ryan Evans na Michael Diouf ikipigwa 96-91 na mabingwa wa Ujerumani Alba Berlin mjini Berlin.

Wafalme hao wa Denmark, ambao walikuwa wamepepeta Rostock Seawolves 96-89 nchini Ujerumani mnamo Septemba 16, waliongoza Berlin kwa alama 47-43 wakati wa mapumziko baada ya kuandikisha alama 27-21 na 20-22 katika robo mbili za kwanza.

Bears iliumizwa zaidi katika robo ya tatu iliyopoteza 30-19 kabla ya kushinda pembamba robo ya mwisho 25-23.

Ongwae, ambaye alikuwa katika kikosi cha Kenya kilichonyakua medali ya fedha kwenye mashindano ya Bara Afrika ya AfroCan 2019 nchini Mali, alifunga alama 11 dhidi ya Berlin, huku QJ Peterson akichangia alama nyingi (23) na kufuatiwa na Diouf (17) na Dentmon (13). Niels Giffey alipachika alama nyingi za Berlin (21).

Timu hiyo ya Bears, ambayo itaelekea nchini Cyprus hapo Septemba 21 kwa mechi za kufuzu kushiriki Klabu Bingwa, ilikuwa imechabanga London Lions 105-88 katika mechi nyingine ya kujipiga msasa mnamo Septemba 6 ilipoalika Waingereza hao nchini Denmark.

Itakabana koo na Hapoel Tel Aviv kutoka Israel katika nusu-fainali ya kwanza ya Kundi A hapo Septemba 23 mjini Nicosia. Ikishinda nusu-fainali hiyo, itakutana na mshindi wa nusu-fainali ya pili kati ya Anwil Wloclawek (Poland) na Belfus Mons-Hainaut (Ubelgiji) katika fainali mnamo Septemba 25.

Bingwa wa kundi hili atatiwa katika Kundi A la Klabu Bingwa linalojumuisha Dinamo Sassari (Italia), Galatasaray Doga Sigorta (Uturuki), Iberostar Tenerife (Uhispania), Peristeri Winmasters (Ugiriki), Rytas (Lithuania), SIG Strasbourg (Ufaransa) na VEF Riga (Latvia).

Isiposhinda mechi za kuingia Klabu Bingwa, Bears itateremka katika ligi ya daraja ya pili (Europe Cup).

TAFSIRI Na GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Fowadi ‘Crucial’ Wasambo kurejea KPL

Kinara wa kampuni ya bima akana kuiba mamilioni